McTominay ajichimbia Old Traford hadi 2023

Muktasari:

  • Kuumia kwa kiungo Fellaini kumesababisha asihamishwe kwa mkopo baada ya kucheza mechi mbili tu chini ya kocha Solskjaer

Manchester. Scott McTominay amesaini mkataba mpya na Manchester United ambao utambakiza Old Trafford hadi mwaka 2023, akiwekewa nafasi ya kuongeza kwa mwaka mmoja zaidi, klabu hiyo ya Ligi Kuu ilisema jana.
"Manchester United imekuwa maishani mwangu tangu nikiwa na miaka mitanoe na kila nilipoichezea nimekuwa nikiungwa mkono na hicho ndicho ambacho nimekuwa nikikitaka," alisema McTominay mwenye umri wa miaka 22 katika taarifa yake iliyotumwa manutd.com.
"Mimi bado ni kijana na wakati wote najifunza kutoka kwa kocha, wasaidizi wake na kundi la wachezaji wa kiwango cha juu duniani," aliongeza McTominay.
McTominay amecheza mechi nane akiwa na United msimu huu, lakini tangui kuwasili kwa Ole Gunnar Solskjaer Desemba amepangwa mechi mbili tu-- wakati waliposhinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Reading katika Koimbe la FA na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tottenham.
Kutopangwa kuliibua ubashiri kuwa angehamishwa kwa mkopo ili aende kupata uzoefu zaidi, lakini kuumia kwa kiungo Marouane Fellaini kumebadili mwelekeo.
Solskjaer alisema mchezaji huyo wa kimataifa wa Scotland anatarajiwa kufanya makubwa kwenye klabu hiyo.
"Amekuwa na klabu hii tangu akiwa na umri mdogo sana. Amepitia katika timu za vijana na katika miaka miwili amefanya mambo mazuri," alisema.
"Ni kiungo kijana na amekuwa akipata ubora zaidi wakati wote. Ni mchezaji mwenye akili na mwenye kutaka kujifunza wakati wote."