Mchongo mpya wa Mo Dewji kuiua AS Vita

Thursday March 14 2019

 

By THOBIAS SEBASTIAN NA THOMAS NG’ITU

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba watakuwa wakisaka hatma yao ya kufuzu robo fainali watakapovaana na AS Vita ya DR Congo.

Mchezo huo ambao joto lake limeanza kupanda mapema, lakini Simba ambayo ipo nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Kundi D wakiwa na pointi sita, wanahitaji ushindi tu ili kufuzu hatua inayofuata huku pia ikiomba mechi ya Al Ahly na JS Saoura iwe na matokeo hata ya sare tu.

Hata hivyo, uongozi wa Simba chini ya bilionea Mohammed Dewji ‘MO’ umekuwa ukitekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa na sasa wameamua kuweka dau la Sh 100 milioni kwa mastaa wake ili kuondoka na pointi tatu kwenye mchezo huo wa mwisho.

Nusanusa ya Mwanaspoti imebaini kuwa, nyota wa Simba mbali na kuwekewa Sh 100 milioni kama wataisambaratisha AS Vita, kila wanaposhinda mchezo katika mashindano yoyote wanapewa posho za maana.

Wachezaji hao wa Simba msimu huu mbali ya kuwekewa pesa hiyo Sh 100 milioni kama wataichapa AS Vita, bado wataendelea kuchota pesa katika mechi za Ligi Kuu Bara ambazo wanashinda.

Ligi Kuu Bara msimu huu Simba watacheza mechi 38 mpaka kumalizika, lakini wachezaji wa kikosi hiko kama watashinda katika mechi yoyote ukiondoa Yanga na Azam wanapewa Sh 10 milioni kama posho.

Katika mechi dhidi ya Azam nyota hao wa Simba waliwekewa Sh 50 milioni baada ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza walichukua posho hiyo, na hata mechi ya mzunguko wa pili pesa kama hiyo itawekwa kama watashinda mechi ya pili.

Nyota hao wa Simba katika mechi dhidi ya watani zao Yanga posho ni tofauti kabisa na nyingine zote kwani, kila moja waliwekewa Sh 100 milioni na ile ya mzunguko wa kwanza waliikosa kutokana kumalizika kwa sare, lakini mechi ya pili waliipata baada ya bao la Meddie Kagere.

MO hataki mchezo sambamba na uongozi wake katika kuona Simba inatisha kimataifa katika kila mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi ambazo wameshinda kati ya zile sita waliweka Sh 100 milioni.

Mbali ya hivyo tayari wachezaji wa Simba walishavuta posho ya Sh 100 milioni katika mechi ya hatua ya mtoani kabla ya kuingia makundi dhidi ya Nkana ya Zambia ambayo walicheza hapa Dar es Salaam huku zile mbili dhidi ya Mbabane Swallows walipewa Sh 70, milioni.

WASIKIE VIONGOZI

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, alisema katika kila mechi wanayoshinda kwenye mashindano hawatoki bure bila ya kupata posho ili kuongeza motisha.

“Hatuwezi kuweka wazi ni kiasi gani cha pesa ambacho kinatolewa kwa wachezaji wetu endapo watashinda mchezo, lakini tunawapatia mbali ya mishahara yao ili kuongeza morali.

“Posho hizo huwa hazifanani kwa wachezaji wote kwani wale ambao, waliocheza wanapata zaidi ya waliokuwa benchi na ambao hawakucheza kabisa,” alisema Magori.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema hakuna mechi yoyote ambayo wachezaji wa Simba wanacheza bila kupata posho kama watakuwa wameondoka na ushindi. “Wachezaji wetu hawa ili kuwajenga katika morali ya kushindana zaidi uongozi umejiwekea utaratibu wa kuwapa posho katika kila mechi ambazo wataondoka na pointi tatu ingawa huwa hazifanani,” alisema Try Again ambaye alikuwa Kaimu Rais katika uongozi iliomaliza muda wake.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Mlamu Ng’ambi alisema uongozi wa wao umeshapanga muundo wa ulipaji posho kwa wachezaji wote ambao upo hadi msimu unamalizika kulingana na mechi husika. “Wanapata posho ambazo zinaongeza morali na hali ya kushindana kwao na kufanya maendeleo ya kimaisha ambazo si vyema kuweka wazi mambo ya pesa hadharani, lakini tunawapa kila wanaposhinda katika mashindano yote ambayo tunashuriki msimu huu,” alisema Ng’ambi.

WASIKIE WACHEZAJI

Nahodha Msaidizi wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alisema hayo mambo ya kupokea posho huwa yanafanyika kwa siri ndani ya klabu yao na si vyema kuweka wazi kwani hata aliye nje ya timu si vizuri kufahamu.

“Hayo mambo ya posho huwa ni ya lawama sana si vyema kuyaweka wazi kwani masuala ya pesa yanaweza kuniweka matatizoni,” alisema Tshabalala.

Advertisement