Mesut Ozil alaumu ukimya kwa Waislamu wa China

Muktasari:

Ozil anasema anashangazwa kwa nchi za Kiislamu kutokemea mateso wanayofanyiwa Waislamu hao walioko jimbo la Xinjiang nchini China.

Istanbul, Uturuki. Mshambuliaji wa Arsenal, Mesut Ozil, Mjerumani ambaye ana asili ya Uturuki, leo Ijumaa ameeleza kuunga mkono jamii ya Uighurs kutoka jimbo la Xinjiang na kulaumu nchi za Kiislamu kwa kushindwa kuwatetea.
"Korani zinachomwa... Misikiti inafungwa ... Shule za Kiislamu zinapigwa marufuku ... Wasomi wa kidini wanauawa moja baada ya mwingine ... Ndugu wanapelekwa kinguvu makambini," Ozil ameandika katika akaunti yake ya Twitter kwa lugha ya Kituruki.
"Waislamu wamekaa kimya. sauti yao haisikiki," aliandika kwenye ukurasa huo ambao nyuma una rangi ya bluu na alama ya mwezi, ambayo ni bendera ya kile ambacho jamii hiyo ya Uighur inaita East Turkestan (Uturuki ya Mashariki).
China imekuwa ikikososlewa na jumuiya ya kimataifa kwa kujenga kambi kadhaa katioka jimbo hilo la Xinjiang kwa lengo la kuwafanya wananchi hao wa Uighur kuwa na utamaduni wa Han ambao unatumiwa na wengi katika nchi hiyo.
makundi ya wapigania haki na watalaamu wanasema zaidi ya watu milioni moja wa kabila hilo la Uighurs na watu wengine kutoka jamii ya Kiislamu ambayo si kubwa wamezungukwa katika kambi hizo zilizo katika jimbo lenye ulinzi mkali.
Baada ya awali kukanusha kuwa hakuna kambi hizo, baadaye China ilizielezea kama shule za ufundi ambazo zinalenga kuwaondoa na Uislamu wa itikadi kali na vurugu.
Uturuki, ambayo imechukua jina lake kutoka watu wa Turkic ambao walihama kutokea barani Asia, ni nyumbani kwa jamii hiyo ya Uighur na mara kwa mara hueleza hofu yake kuhusu hali ilivyo katika jimbo la Xinjiang.
Katika ujumbe wake wa Twitter, Ozil alisema mataifa ya Magharibi nas vyombo vya habari vimeweka suala la watu wa Uighur katika ajenda zao na kuongeza kusema: "Kitakachokumbukwa miaka kadhaa baadaye si mateso yanayotolewa na watesaji bali ukimya wa Waislamu wenzao."
Arsenal ilijitenga na maoni hayo ya Ozil ikiwa ni jitihada za kuepuka kuingia katika mzozo na China, ambako klabu hiyo ina mipango ya kibiashara.
"Ujumbe uliochapishwa ni maoni binafsi ya Ozil," ilisema klabu hiyo kwa lugha ya Kichina katika akaunti ya klabu hiyo ya Weibo ambayo ni kama Twitter.
"Kama klabu ya soka, Arsenal imekuwa ikiheshimu kanuni za kutojihusisha na siasa.”
Lakini mashabiki wachache wenye hasira nchini China walipendekeza kutorushwa hewani kwa mechi zinazomuhusisha Ozil.
"Natumaini watapiga marufuku mechi zinazomuhusu Ozil na shughuli za biashara (nchini China)," aliandika mmoja wa watumiaji wa Weibo.
Shabiki mwingine Mchina alisema alilia usiku baada ya kusoma ujumbe huo ambao mwanasoka huyo nyota pia aliutuma katika akaunti yake ya Instagram.
"Kwa zaidi ya miaka kumi, nimevaa jezi ya Arsenal yenye namba ya Ozil. Hiyo haitatokea tena," aliandika katika akaunti yake ya Weibo.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 aliibua utata mwaka jana wkati alipopiga picha na rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, akiibua maswali kuhusu utiifu wake kwa Ujerumani baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018.
Baadaye Ozil alitangaza kujiuzulu kuchezea timu ya taifa, akiwatuhumu viongozi wa soka wa Ujerumani kwa ubaguzi. Erdogan alikuwa mpambe wa Ozil wakati alipooa jijini Istanbul mapema mwaka huu.