Mgogoro wafukuta Kamisheni ya Ngumi TPBRC

Aliyekuwa rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah

Dar es Salaam.Hali si shwari ndani ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), kutokana na mpasuko wa kiuongozi ulioibuka ndani ya chombo hicho.

Chanzo cha mgogoro ndani ya kamisheni hiyo inadaiwa kimetokana na uongozi kutofuata Katiba ya TPBRC kutekeleza majukumu yake ya kiutendaji.

Aliyekuwa rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah ‘Ustadhi’ anadaiwa ndiye chanzo cha mgogoro ulioibua makundi mawili yanayokinzana kuhusu utendaji wa kamisheni.

Akizungumza Dar es Salaam, promota wa ngumi Shomari Kimbau alidai Ustadhi ni chanzo cha mgogoro kwa kuwa amekuwa akifanya kazi za kamisheni wakati si kiongozi.

“Ustadhi ndiye tatizo amekuwa kama kiongozi, kila anachosema yeye kamisheni inafuata rais (Joe Anea) anamsikiliza sababu alimsaidia wakati wa uchaguzi, ” alidai Kimbau.

Wakati Kimbau akitoa tuhuma hizo, Ustadhi alidai hana mamlaka ya kufanya kazi za kamisheni kwa kuwa si kiongozi. Alisema amekuwa akitoa elimu kwa wengine kuhusu majukumu ya kamisheni na mwenendo wa mchezo wa ngumi nchini, lakini kwa kufuata Katiba.

“Siko katika kamisheni, si kiongozi na sitaki kuwa msemaji wa kamisheni watu wanaodhani nafanya majukumu ya kamati wanakosea,” alisema Ustadhi.

Kauli TPBRC

Akizungumzia madai hayo, Anea alisema kamisheni haiwezi kufuata matakwa ya Ustadhi kama inavyodaiwa na baadhi ya wadau wa ngumi.

“Wadau watuache tufanye kazi na matunda watayaona siku si nyingi, kama nilivyosema, lengo ni kuondoa makundi na kurejesha heshima ya ngumi za kulipwa,” alisema Anea.

Kauli za wadau

Akizungumzia mgogoro ndani ya kamisheni hiyo, bondia nyota wa zamani nchini Koba Kimanga alisema tatizo linalochangia kudumaza mchezo wa ngumi za kulipwa ni wadau kutotaka kutokubali ukweli.

Rais wa PST, Emmanuel Mlundwa alidai jitihada za Serikali kumaliza migogoro katika ngumi za kulipwa zinakwamishwa ni Ustadhi, lakini akashauri kamisheni iliangalie kwa jicho la tatu na isikubali kuchafuka sababu ya urafiki.

Tamko la Serikali

Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Nchini, Yusuph Singo alisema Serikali itachukua hatua ikibaini kuna mgogoro ndani ya kamisheni hiyo kwa kuwa lengo la kuunda chombo hicho ni kuondoa migogoro.