Mhasibu Simba aeleza Aveva alivyotumia fedha za Okwi

Muktasari:

Shahidi huyo alidai kwa kawaida fedha zote zinazotolewa katika akaunti ya klabu ya Simba kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya klabu hiyo, hujadiliwa na Kamati ya Utendaji

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Klabu ya Simba, Amos Gahumeni (39) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jinsi aliyekuwa rais wa klabu hiyo Evans Aveva na wenzake, walivyotumia fedha za ada ya uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kwa matumizi yao binafsi.

Guhumeni ameieleza mahakama hiyo leo, Juni 26, 2019 wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya vigogo watu wa klabu ya Simba aliyekuwa rais Aveva, Makamu wa wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Shahidi huyo alidia kuwa, Klabu ya Simba ililipwa jumla ya Dola za kimarekani 319, 212 na Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia ikiwa ni ada ya uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kwenda klabu hiyo ya nchini Tunisia.

Guhameni alidai kati ya fedha hizo zilizolipwa na klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia, dola 300,000 zilihamishiwa katika akaunti ya mshtakiwa Aveva bila kujadiliwa katika kikao cha Kamati Utendaji ya Klabu hiyo.

Akiongozwa na wakili wa Takukuru, Leonard Swai, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, shahidi huyo alidai kwa kawaida fedha zote zinazotolewa katika akaunti ya klabu ya Simba kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya klabu hiyo, hujadiliwa na Kamati ya Utendaji, kabla ya kuzitoa fedha hizo kwa ajili ya shughuli za klabu hiyo

Kesi bado inaendeelea.