Mhilu hayupo Simba, Yanga anawaza nje

Mwanza. Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Yusuph Mhilu amesema kwa sasa kipaumbele chake si kuzichezea Simba au Yanga, bali kucheza soka la kulipwa nje ya nchi msimu ujao na kwamba mipango inaenda vizuri.

Mchezaji huyo mwenye mabao 11 katika Ligi Kuu na matatu ya Kombe la Shirikisho (FA), amekuwa na msimu mzuri kutokana na kiwango bora alichoonesha akiwa na timu yake.

Mhilu ambaye aliibuliwa na Yanga kabla ya kujiunga na Ndanda msimu uliopita, ameiwezesha Kagera Sugar kuwa ya nane ikiwa na pointi 41 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Alisema kwa kiwango alichoonesha msimu huu, anafikiria kusaka maisha mapya nje ya Tanzania.

Alisema ameshaanza mipango chini ya msimamizi wake na huenda msimu ujao akawa katika moja ya timu ya nje ya nchi akisema suala la masilahi halimuumizi kichwa, bali anataka nafasi ya kucheza.

“Hakuna asiyezipenda Simba na Yanga, lakini mimi nimeshecheza mojawapo kwa hiyo najua changamoto zake, kwa sasa nafikiria zaidi kucheza soka nje ili kupanua wigo kwenye kazi yangu,” alisema Mhilu.

Hata hivyo, alisema iwapo mipango yake ya kukipiga nje ya nchi itakwama, atabaki Kagera Sugar.

Alisema janga la virusi vya corona limemtibulia mambo mengi na kubainisha kuwa kwa kipindi hiki ambacho shughuli za michezo zimesimama, ataendelea kujifua ili ligi ikiendelea aweze kurejea akiwa katika ubora wake.