Mkenya afurahia kuandika historia ya marathoni

Muktasari:

  • Kipchoge amefanikiwa kumaliza mbio za marathoni akitumia chini ya saa mbili, jambo ambalo alishindwa kulifanya mwaka 2017.

Mwanariadha wa Kenya, Eliud Kipchoge leo Jumamosi ameandika historia baada ya kuondoa kikwazo cha kumaliza mbio za marathoni kwa masaa mawili na kusema amefurahi kuwaambia watu kuwa hakuna ukomo kwa binadamu.
Huku mishale ya saa ikisomela saa 1 dakika 59 na sekunde 40.2, bingwa huyo wa Olpimiki amekuwa binadamu wa kwanza duniani kumaliza mbio za marathoni chini ya muda uliozoeleka wa saa mbili za zaidi baada ya kufanya hivyo katika eneo la Prater Park.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 34, tayari anashikilia rekodi ya dunia ya marathoni ya saa 2:01:39 ambayo aliiweka katika mbio za Marathoni za Berlin Septemba 16, 2018.
Lakini akisindikizwa na wanariadha 41 na mbele kukiwa na gari kwa ajili ya kumfanya akimbie zaidi, Kipchoge aliboresha muda wake na hivyo kufuta makosa ya jaribio lake la kwanza aliloshindwa kufikia muda huo miaka miwili iliyopita jijini Monza, Italia.
"Nimejaribu na ni mtu mwenye furaha kukimbia chini ya saa mbili ili kuhamasisha watu wengi, kuwaambia watu kuwa hakuna binadamu mwenye ukomo," alisema Kipchoge.
"Nategemea wanariadha wengi zaidi kote duniani kukimbia chini ya saa mbili baada ya hili la leo."
Alisema kitendo cha kukaribia sehemu ya kumalizia ni "wakati bora kuliko mwingine wowote katika maisha yake".
Akikimbia kwa kasi ya dakika 2:50 kwa kilomita, Kipchoge alivuka mstari wa kumalizia mbio hizo akitabasamu na kuonyesha ishara ya ushindi.
Bilionea Muingereza Jim Ratcliffe, ambaye ni muasisi wa mdhamini mkuu wa tukio hilo ambao ni Ineos, alionyesha kuvutiwa na jambo hilo na huw aanashiriki riadha ya michezo tofauti.
"Kilomita ya mwisho ambayo alionekana kuongeza kasi alionekana mtu asiye wa kawaida," alisema Ratcliffe.
Kipchoge alikuwa ameshakuwa mbele kwa sekunde 11 wakati mashabiki wakikusanyika kwenye eneo la kukimbilia, wengi wao wakipunga bendera ya Kenya, na wakishangilia kwa sauti.
Koch wake, Patrick Sang, alisema Mkenya huyo "ametuhamasiasha wote kwamba tunaweza kujitanua kupita ukomo katika maisha yetu".
"Rekodi zinawekwa ili zivunjwe, kwa hiyo mtu mwingine atajaribu tena, lakini historia imewekwa. Ni kitu usichoweza kuamini," aliongeza Sang.
Kipchoge aliwaambia waandishi wa habari mapema wiki hii mjini Vienna kuwa jaribio lake katika mji huo mkuu wa Austri ni "kuandika historia duniani, kama mtu wa kwanza kwenda mwezini".

- Inafurahisha' -
Kutokana na jinsi mbio hizo zilivyoandaliwa na kasi kuongezwa, Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) halitatambua muda wa Kipchoge kuwa ni rekodi ya dunia.
Sehemu aliyopkimbilia ilitengenezwa na yaliwekwa mazingira mengine kama kona ambazo zingeweza kupunguza muda na kuepuka majeraha.
Waongezaji kasi (pacemakers) waliamua kumsaidia wakati wote wa mbio hizo za kilomita 42.195. Walioshiriki ni pamoja na bingwa wa Olimpiki wa mbio za mita 1,500, Matthew Centrowitz na bingwa wa zamani wa dunia, Bernard Lagat.
Sehemu ya kukimbilia inahusisha kilomita 4.3 zilizonyooka, ambazo Mkenya huyo alikimbia kwa kupanda na kushuka katika siku hiyo iliyokuwa kavu.
Mashabiki kadhaa walimshangilia Kipchoge kila alipopita.
William Magachi, 33, kutoka Nairobi, alikuwa mmoja wa Wakenya waliokuwa wakimuangalia.
"Inafurahisha. Ni mtu asiye wa kawaida, mtu mwenye kuona lolote linawezekana, amefanya kile alichoweza," alisema.
"Amevunja rekodi. Haijawahi kutokea na inawezekana isitokee maishani mwangu…. mimi ni mtu mwenye bahati."
Kipchoge alijaribu kufanya hivyo Mei mwaka 2017 alipokimbia kwenye bustani ya Monza National Autodrome nchini Italia, lakini akashindwa kwa sekunde chache alipotumia saa 2:00:25.