Mkono wa Yondani, Ajibu wazua jambo

Dar es Salaam. Kitendo cha beki Kelvin Yondani kugoma kumpa mkono Ibrahim Ajibu, kimeibua mjadala kwa baadhi ya wachezaji nyota wa zamani wa Yanga.

Yondani aliyempa kitambaa cha unahodha Ajibu, hakumpa mkono kiungo huyo wakati akiwatambulisha wachezaji wa Yanga mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima alisema Yondani alipaswa kumpa mkono Ajibu bila kujali kama alikuwa sahihi au vinginevyo.

Hata hivyo, alisema Ajibu hakuwa sahihi kutambulisha wenzake kwa kuwapa mkono kwa kuwa siyo jambo la kawaida nahodha kuwatambulisha wachezaji wenzake kwa kuwapa mkono. Nguli mwingine wa Yanga, Peter Tino alisema ameona tukio hilo ni utovu wa nidhamu kwa Yondani akidai hata kama mwenzake alikosea hakupaswa kuonyesha kitendo hicho mbele ya mgeni rasmi.

Mchambuzi wa soka Ally Mayay alisema kitendo cha Yondani kugomea mkono wa Ajibu si tukio la kuibua mjadala ingawa baadhi ya watu wanaweza kuhisi kuna tatizo baina yao.

Akizungumza jana , Ajibu alisema anadhani wachezaji wenzake walimshangaa kuwatambulisha kwa kuwashika mikono kwa kuwa mara nyingi hawafanyi hivyo. “Si kaka yangu Yondani pekee aliyesita kunipa mkono, Dante pia, Yondani aliniambia hii mpya,” alisema Ajibu.