Simba yathibitisha kuwaita Mkude, Chama, Nyoni kwa utovu wa nidhamu

Muktasari:

Wachezaji hao walikuwa nje ya timu kutokana na sababu ambazo bado hazijajulikana na wameingia kambi ya timu ya taifa na kuendelea na majukumu yao kama kawaida.

Dar es Salaam.Uongozi wa Simba umesema hatma ya wachezaji wake Jonas Mkude, Gadiel Michael, Erasto Nyoni na Clatous Chama itajulikana baada ya michezo ya timu za taifa.

Wachezaji hao wanatuhumiwa kwa makosa utovu wa nidhamu baada ya kushindwa kusafiri na timu kwenda Kanda ya Ziwa kati michezo miwili dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ilisema klabu ilifanya kikao cha ndani cha nidhamu na wachezaji hao Oktoba 3 mwaka huu.

"Kikao hicho kilijali usawa na haki ambapo walalamikiwa walitakiwa kujieleza na mashahidi waliitwa ili kutoa ushahidi wao kuhusiana na sakata hilo," ilisema taarifa hiyo.

"Kutokana na mchakato huo klabu iliteua kamati huru ya nidhamu inayoungwa na wanasheria wanne kushughulikia suala hilo, kuhakikisha mchakato unakuwa na usawa na haki baada ya kumaliza kazi hiyo kamati itawasirisha ripoti kwa mtendaji mkuu."

Taarifa hiyo ya Senzo ilisema klabu inasubiri wachezaji hao wamalize majukumu ya timu ya taifa kisha kukutana nao ili kumaliza sakata hilo.

Awali Kocha wa Simba, Patrick Aussems ameshikilia msimamo wake baada ya kuwaondoa katika kikosi wachezaji hao waandamizi bila kujali umuhimu wao ndani ya klabu hiyo.

Wachezaji hao ni Mkude, Nyoni, Michael na Chama hawajafanya mazoezi na kikosi hicho kwa siku 14.

Aussems amegoma kuwapokea nyota hao wa kikosi cha kwanza kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Mkude, Nyoni na Chama wanadaiwa kukutwa wamekunywa pombe ambapo walichelewa safari ya kwenda Bukoba kuikabili Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara walioshinda mabao 3-0 Septemba 26.

Gadiel anadaiwa hakuripoti kambini baada ya kumaliza majukumu ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’.

Pia wachezaji hao walikosa mchezo uliofuata dhidi ya Biashara United walioshinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Karume, mkoani Mara.

Mmoja wa viongozi wa Simba aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema Aussems amegoma kuwapokea wachezaji hao kwa utovu wa nidhamu.

“Mwalimu amegoma kuwapokea wachezaji wote wanne kwasababu ana ushahidi wa kutosha kuhusu vitendo vyao vya utovu wa nidhamu. Amepeleka shauri lao kwa Mtendaji Mkuu kwa hatua zaidi,”kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilidai wachezaji hao walihojiwa na Mtendaji Mkuu Senzo Masingiza na Aussems kuhusu makosa yao ambapo kila mmoja alitakiwa kujitetea kabla ya kuchukuliwa hatua.

Wakati Nyoni alidai alikuwa akiuguliwa na mwanaye, Gadiel alidai alikuwa na maumivu, lakini hata hivyo utetezi wao umeonekana kugonga mwamba na wanasubiri kuchukuliwa hatua.

Chanzo hicho kilidai Mkude na Chama wanaweza kuchukuliwa hatua zaidi kwa kuwa makosa yao yanadaiwa yamekuwa yakijirudia kulinganisha na Nyoni, Gadiel. “Ni vyema wapewe adhabu ili iwe fundisho na wajitambue kwani wanaweza kuigharimu timu au kuipa sifa mbaya klabu,”alisema kigogo huyo ambaye ni mjumbe wa bodi.

Aussems alipoulizwa kuhusu sakata la wachezaji hao alijibu kwa kifupi:” Mkude na wenzake wako timu ya Taifa”.

Kwa upande wake Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema suala hilo lipo kwa uongozi wa juu na hawezi kuzungumza.

Mtendaji Mkuu alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa jambo hilo alimtaka mwandishi kumtumia maswali kwa barua pepe, lakini hakutoa ushirikiano licha ya kutumiwa kama alivyoagiza na hata alipotafutwa kwa simu.

Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda alisema hawana taarifa za utovu wa nidhamu wa Mkude, Nyoni, Gadiel na wanaendelea na mazoezi kama kawaida.