Mkwabi avunja ukimya Simba

Muktasari:

Kisha ikaelezwa Mo Dewji alitishia kujitoa klabuni hapo akitambuliwa kama mwekezaji kwa madai anahujumiwa na Mkwabi, kwa vile mambo mengi hatakelezi kwa wakati na kurudisha nyuma maendeleo ya klabu kwa kushindwa kukamilika mchakato wa uwekezaji.

WAKATI Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) ikimruka aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Simba, Hamis Kilomoni, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Swedy Mkwabi amevunja ukimya juu ya sakata lililopo ndani ya klabu hiyo.
Ipo hivi. Kwa siku za karibuni kumekuwa na sintofahamu Msimbazi baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed ‘Mo’ Dewji kuandika jumbe zenye utata katika kurasa zake za mitandao ya kijamii na kuzua maswali mengi kwa wadau wa soka.
Kisha ikaelezwa Mo Dewji alitishia kujitoa klabuni hapo akitambuliwa kama mwekezaji kwa madai anahujumiwa na Mkwabi, kwa vile mambo mengi hatakelezi kwa wakati na kurudisha nyuma maendeleo ya klabu kwa kushindwa kukamilika mchakato wa uwekezaji.
Mo Dewji katika ujumbe wake amekuwa akionyesha kutokuwa na amani ndani ya Simba, kabla ya kuelezwa na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kuwa, Mkwabi anaonekana tatizo na hasa ukaribu wake na Mzee Kilomoni anayeshikilia hati za jengo ya klabu hiyo.
Taarifa zikaongeza kuwa, Mo Dewji alikuwa tayari kuondoka Simba, huku akisisitiza hatazidai Sh 5 bilioni alizotumia hadi sasa ndani ya klabu hiyo na kwenda mbali zaidi kutaka kuitisha mkutano wa dharura wa wanachama ili watoe uamuzi wao.
Majuzi ikatolewa taarifa kuwa, kwenye kikao cha pamoja cha bodi, wawili hao kila mmoja alifunguka yake na mambo kumalizika kwa kuzika tofauti kabla ya Mo Dewji kuweka tena ujumbe tata na kuzagaa taarifa kwa kwamba Mkwabi alikuwa akijiandaa kujiuzulu.
Lakini Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Crescentius Magori alizungumza na vyombo vya habari Jumanne na kueleza walivyomfutilia mbali Kilomoni na kwamba hawamtambui kama Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini na kuonyesha barua kutoka RITA.
Hata hivyo, jana Mwanaspoti liliamua kumsaka Mkwabi ili angalau afafanue kinachoendelea juu yake na mustakabali wa Simba kwa ujumla, naye akafunguka japo kwa ufupi, tena baada ya kulazimishwa sana kwani alikuwa akisititiza Simba kila kitu ni shwari.
Mkwabi alisema hana taarifa rasmi za tuhuma zote dhidi yake zaidi ya kuzisikia na kuzisoma kama wengine na kusisitiza mbona anafanya kazi vizuri tu na wenzake Simba.
“Hakuna taarifa niliyopewa rasmi kuwa namhujumu Mo Dewji, nazisikia na kuzisoma tu, ninachofahamu mimi ni kwamba ndani ya Simba hakuna tatizo lolote hadi sasa na kama kuna tatizo basi litawekwa wazi na ndipo hapo nitakajua ni kitu gani namhujumu.
“Vinginevyo sina tatizo na Mo Dewji na sina uwezo wa kumhujumu, tuna mawasiliano mazuri na kazi zinafanywa kama kawaida ndani ya Simba. Kuhusu suala la kujiuzulu basi sijafikiria, hilo huenda litafikiriwa endapo tu nitapewa taarifa rasmi kuwa namhujumu tena kwa ushahidi kisha nitatafakari na kutoa uamuzi, ila kwa sasa hakuna kinachoendelea.”
Mkwabi alisema kama kiongozi mkuu wa Simba anajua wajibu wake na anatambua suala la Simba kuendeshwa kisasa, lakini kama kweli yeye ni kikwazo afahamishwe ili ajipime kwani amepewa dhamana na wanachama waliomchagua kwenye Uchaguzi Mkuu.

RITA YAMRUKA KILOMONI
Katika hatua nyingine wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Klabu ya Simba, Hamis Kilomoni akijipanga kufyatua mabomu Msimbazi na kutolea ufafanuzi juu ya kupigwa kwake chini, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imesema haina taarifa za nyota huyo wa zamani wa soka, kuwa mdhamini wa klabu hiyo.
Rita ilienda mbali zaidi na kueleza hakuna rekodi inayoonyesha Kilomoni kama bado yupo kwenye nafasi hiyo kwa sasa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Rita, Josephat Kimaro alisema taarifa walizonazo Rita zinawatambua wadhamini wanne lakini Kilomoni si miongoni mwao.
“Rekodi zetu tangu Novemba 2017 zinaonyesha wadhamini wa Simba ni Ramesh Patel, Abdul Abbas, Idd Mgoyi na Profesa Juma Kapuya,” alisema Kimaro.
Alipoulizwa taratibu ambazo zinafanyika hadi mdhamini kuondolewa, Kimaro alisema zimewekwa kwenye mtandao wa Rita ambao ni www.rita.go.tz.
Katika mtandao kipengele cha mabadiliko ya chombo, jina au marekebisho ya mdhamini kinasema lazima kuwalisha nakala iliyothibitishwa ya kumbukumbu ya mkutano uliothibitishwa ambao ulifanya mabadiliko ya jina na kurejesha cheti halisi cha zamani.
Kifungu kingine kinaeleza Hairuhusiwi kumiliki ardhi au haki kwenye ardhi, bila kupata kibali cha maandishi kutoka kwa Msimamizi Mkuu wa wadhamini (Kabidhi Wasii Mkuu). Kumtaarifu Msimamizi Mkuu wa wadhamini juu ya mabadiliko yoyote, mabadiliko ya wadhamini, jina la chombo, anwani ya posta, Katiba ndani ya mwezi mmoja.
Akizungumzia barua iliyoonyeshwa juzi Jumanne na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, Kimaro alisema ni barua halali kutoka Rita.
“Ni kweli ile ni barua yetu na kwenye kumbukumbu zetu huku Rita Patel, Abbas, Kapuya na Mgoyi ndiyo wadhamini wa Simba, kwa wengine sifahamu kumbukumbu za nyuma zilikuwa vipi, ila kuanzia Novemba 2017 hao ndiyo wanasomeka kwetu,” alisema Kimaro.
Kimaro alisema tangu Novemba 2017 Rita haijapata malalamiko yoyote ya mtu au watu kupinga kuhusu mabadiliko hayo ya wadhamini.

KILOMONI HUYU HAPA
Lakini Kilomoni alipotafutwa ili kuzungumzia alisema kuna taratibu za kumuondoa mdhamini na si ambavyo Simba inataka kufanya, hasa baada ya Magori kusema klabu hiyo imefunga mjadala wa Kilomoni, kwani si mdhamini tena wa klabu yao na wako mbioni kumshtaki kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Alisema Kilomoni amekuwa akijitambulisha kama Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini huku akijua si kweli na anafanya kimakosa.
Kilomoni alipoulizwa juu ya kutotambuliwa na Rita kuwa miongoni mwa wadhamini wa Simba alisema atatolea ufafanuzi suala hilo Jumatatu ya wiki ijayo.
“Mambo ya Simba nitayazungumzia wiki ijayo, lakini bado natambua mimi ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, kuna taratibu za kuniondoa sivyo wanavyotaka kufanya, siwezi kung’ang’ania kama uongozi wa Simba na wanachama utaamua na kuridhia, ila sivyo anavyosema Magori. Kwanza huyo Magori ni nani ndani ya Simba hata aamue hivyo?”
Chini ya uongozi wa Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ iliwahi kutangaza kumfungia Kilomoni katika mkutano wa wanachama uliofanyika Dar es Salaam na kutangaza kumfuta uanachama kama hatofuta kesi mahakamani, lakini akaibukia kwenye uchaguzi mkuu wa klabu hiyo na kushangiliwa na baadhi ya wanachama.