Mkwasa, Kibadeni waipa Stars mchongo wa kuiua Senegal

Wednesday June 19 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Wakati timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ ikijiandaa kwa mechi ya ufunguzi dhidi ya Senegal, imepewa mambo matatu makubwa ambayo yataipa matokeo chanya dhidi ya wapinzani wao.

Taifa Stars itatupa karata ya kwanza katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), zinazofanyika Misri dhidi ya Senegal, Jumapili wiki hii.

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Emmanuel Amunike ilicheza mechi mbili za kimataifa za kirafiki ambapo ilifungwa bao 1-0 na Misri kisha juzi usiku ikatoka sare 1-1 na Zimbabwe.

Matokeo ya Taifa Stars ya mechi hizo mbili yametolewa maoni tofauti na makocha nguli akiwemo Charles Mkwasa aliyewahi kuinoa timu hiyo kwa nyakati tofauti.

Mkwasa alitaja mambo makubwa matatu aliyodai endapo yatafanyiwa kazi kikamilifu, Taifa Stars inaweza kufanya maajabu dhidi ya Senegal.

Mkwasa aliyataja mambo hayo yanayoweza kuibeba Taifa Stars kuwa ni nidhamu ya mchezo, kujiamini na kupunguza makosa katika muda wote wa dakika 90.

Advertisement

“Wachezaji wawe na nidhamu ya ukabaji, wapunguze makosa ya kizembe na wajiamini, wakifanikiwa katika hilo nafasi ya kufanya vizuri ipo,” alisema.

Alisema mechi mbili ilizocheza Taifa Stars dhidi ya Misri na Zimbabwe zimetoa taswira kwamba timu hiyo ina nafasi nzuri ya kufanya vyema katika mechi za fainali hizo zinazotarajiwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19.

Alisema kila mchezaji anatakiwa kutambua majukumu aliyopewa na benchi la ufundi kwa kuwa mechi ya kwanza katika mashindano ni muhimu kushinda ili kutengeneza mazingira bora katika mechi zinazofuata.

Wakati Mkwasa akitoa maoni hayo, aliyewahi kuwa kocha wa Simba na Taifa Stars, Abdallah Kibadeni alisema dakika 20 za mwanzo ni muhimu kwa timu kuhakikisha hairuhusu bao ambalo linaweza kuwatoa mchezoni wachezaji.

Kibadeni alisema kitendo cha Taifa Stars kufungwa bao 1-0 na Misri kimetoa taswira kuwa wachezaji wamekomaa kwa mashindano makubwa.

“Misri ilikuwa ni timu inayotufunga mabao mengi, lakini  kufungwa bao 1-0 tena wakiwa kwao kimeonyesha namna Stars ilivyoanza kuimarika,’’ alisema Kibadeni.

Alisema Kocha Amunike anatakiwa kupanga ngome imara itakayocheza kwa nidhamu kwa kuwa Senegal ni timu bora barani Afrika inayoundwa na wachezaji mahiri wengi wao wakiwa wanacheza soka la kulipwa barani Ulaya.

Kocha wa Prisons, Mohammed Rishard ‘Adolf’ alisema kiwango bora cha Taifa Stars dhidi ya Misri na Zimbabwe kinaweza kuipa tabu Senegal Juni 23.

“Mechi za kirafiki zimeonyesha wachezaji wamejenga mtiririko mzuri wa ushindi, kama watacheza kwa nidhamu na kujiamini wanaweza kufikia malengo ambayo Kocha Amunike na Watanzania tunayahitaji,” alisema Rishard.

Taifa Stars imepangwa Kundi C dhidi ya Senegal, Kenya na Algeria. Mara ya mwisho Tanzania kucheza fainali hizo ilikuwa mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria.

Advertisement