Mkwasa awapa mchongo Yanga

Dar es Salaam. Yanga imepewa mbinu tatu ambazo zitainasua katika wimbi la mtikisiko wa kiuchumi na kuirejesha klabu hiyo katika mstari.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga, Charles Mkwasa alisema klabu hiyo inapitia kipindi kigumu licha ya kupata matokeo mazuri katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, alitaja mambo matatu yanayoweza kuivusha klabu hiyo kuwa ni kufanya uchaguzi ili kupata viongozi halali ambao wataisimamia kikamilifu.

“Kwanza wakubali kufanya uchaguzi, wajaze nafasi za viongozi zilizokuwa wazi ili wapate uongozi thabiti,” alisema Mkwasa.

Mkwasa alisema baada ya uchaguzi, uongozi mpya unapaswa kufanya mabadiliko ya kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu kutoka umiliki wa wanachama kwenda katika kampuni.

Katibu Mkuu huyo wa zamani alitaja jambo la tatu ni kuboresha Katiba ya Yanga ambayo itakuwa dira ya klabu katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiutendaji.

“Mtu yeyote apewe nafasi kuwekeza, kabla ya kuelekea katika shea wafanye maboresho ya Katiba yao ambayo ina kipengele kinasema ndani ya klabu ya Yanga kuwe na kampuni.

“Hii ya kufungua kampuni Yanga italeta fitina watagombana tu, cha kufanya warekebishe Katiba ili yenyewe iwe kampuni, hii itasaidia klabu iwe salama,”alisema Mkwasa.

Alisema Yanga imeingia katika mtikisiko wa kiuchumi kutokana na kuwa na vyanzo vichache vya mapato ambavyo vimeshindwa kutosheleza mahitaji ya klabu.

“Mimi wakati naingia Yanga nilikuta deni la mishahara ya kama miezi miwili, nikiwa na siku tano tu ofisini, ndipo mwenyekiti akaanza kukutana na matatizo.

“Tukaona ili kuisaidia Yanga lazima tupate udhamini, tukaingia udhamini na SportPesa ambayo ilikuwa ikitoa fedha kila baada ya miezi mitatu ambazo zilitusaidia katika utekelezaji wetu wa majukumu ya kiutendaji,” alisema Mkwasa.

Licha ya kupatwa na mtikisiko wa kiuchumi, Yanga inafanya vyema katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo inaongoza kwa pointi 53 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 40 na Simba inafuatia kwa pointi 33.