Mmeskia? Eti huyu haaland anasema hayupo fiti

DORTMUND, UJERUMANI . MMEMSIKIA Erling Haaland huko? Usiku wa juzi Jumanne alipiga mbili kuizamisha Paris Saint-Germain ya Neymar na Kylian Mbappe kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya 16 bora kwenye Ligi Kuu England, kisha akadai ndo kwanza anaanza, bado hayupo kwenye ubora wake.

Straika Haaland amevunja rekodi nyingine katika mechi zake za kwanza huko Borussia Dortmund baada ya kufunga mabao mawili kwenye mechi moja kwa mara ya pili alipowazamisha PSG.

Kinda huyo wa Norway sasa amefunga mabao 11 katika mechi saba za mwanzo alizoichezea Dortmund tangu aliponaswa kwa ada ya Pauni 17 milioni kutokea RB Salzburg na hivyo kumfanya awe amefikisha mabao 35 msimu huu.

Na jambo hilo limemfanya afikishe mabao 10 kwa haraka kwenye Bundesliga kuliko mchezaji yeyote kwenye historia ya michuano hiyo, huku akiwaacha hoi wengi akidai bado hayupo kwenye ubora wake. Haaland alisema: “Nimefurahi kwa tuzo ya mchezaji bora wa mechi, lakini najiona kabisa bado sipo kwenye ubora wangu. Napaswa kucheza kwa kiwango bora zaidi, hivyo nafanyia kazi jambo hilo kuboresha kiwango.

“Matokeo haya tuliyopata bado ni hatari, kwa sababu PSG ni timu yenye nguvu, hivyo bado wana nafasi ya kusonga mbele kwenye mechi ya marudiano.”

Mabao hayo mawili ya Haaland yameifanya Dortmund kushinda 2-1, lakini bao la Neymar limeifanya PSG ya Thomas Tuchel, aliyerudi kukubana na timu yake ya zamani kuwa na faida ya bao la ugenini jambo ambalo atalitumia kwenye mechi ya marudiano huko Parc des Princes.