Mnamibia Yanga aanza kwa mbio kambini Moro

Muktasari:

  • Urkhob awali alikuja nchini mwaka jana na kufanya majaribio katika kikosi cha Simba, huku akicheza michezo kadhaa.

Morogoro. Mshambuliaji mpya wa Yanga, Mnamibia Sadney Urkhob ametua mazoezini na kupokewa na dozi ya mazoezi ya mbio huku akigusa mpira kidogo.

Sadnye aliyewasili jana nchini na kusafirishwa moja kwa moja kuelekea Mkoani Morogoro ilipo kambi ya timu hiyo ameanza mazoezi haraka leo asubuhi.

Mshambuliaji huyo ameonekana akipewa maelekezo ya mazoezi yake na kocha Noel Mwandila akimtofautisha na wengine katika mazoezi hayo.

Mnamibia huyo amekuwa akikimbia peke yake kwa kasi ndogo huku wenzake ambao walimtangulia wakitokea timu ya taifa wakikimbia mbio za kasi tofauti.

Hata hivyo baadaye mshambuliaji huyo alijumuishwa na wenzake katika mazoezi ya pamoja na wenzake ya kuchezea mpira kidogo kisha kufunga mazoezi hayo.

Mshambulaji huyo ameonyesha uwezo mzuri katika kumiliki mpira na kutoa pasi huku akijaribu kuzoeana haraka na wenzake kwa kuelekezana nao.

Urikhob kwa timu zote alizocheza amefunga jumla ya magoli 56, baada ya kucheza, Amazulu(South Afrika)- 2013-2014 mechi 20 na magoli tisa, Saraburi (Thailand) 2015 mechi 30 magoli 12, 2016-2017 Super Power Samut Prakan (Thailand) 2016-2017 mechi 42 na magoli 15, Police Tero Football Club (Thailand) mechi 17 na magoli 6 , PSMS Medan (India) mechi 11 na goli 1 huku Tura Magic akiifungia magoli 13.