Molinga, Balinya waionyoosha JKT

Friday November 22 2019

 

By THOMAS NG'ITU

TIMU ya Yanga imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo Yanga walipata mabao yote kipindi cha kwanza huku mshambuliaji Juma Balinya akiwa amefungua ukurasa wake wa mabao kwenye ligi hiyo.
Yanga ilianza kupata bao la kwanza dakika ya 10 kupitia Patrick Sibomana,  Balinya akifunga bao la pili 21 wakati David Molinga akifunga dakika 34 huku mabao ya JKT Tanzania yakifungwa na Adam Adam dakika 13 na Dany Lyanga dakika 45.
Kipindi cha pili, Yanga ilifanya mabadiliko dakika 50 kwa kumtoa Mapinduzi Balama nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Issa 'Banka'.
Dakika 51, Juma Abdul alionyeshewa kadi ya njano baada ya kumfanyia faulo Adeyum Ahmed.
Kocha wa Yanga, Boniface Mkwasa alifanya badiliko lingine kwa kumtoa Molinga na kuingia Abdulaziz Makame, wakati huo huo JKT  nao walimtoa Richard Maranya nafasi yake alichukuliwa na Hafidh Mussa.
Mabadiliko ya JKT Tanzania chini ya kocha wao Mohamed Abdallah 'Bares' yalionyesha kwenda kuongeza nguvu eneo la kiungo sawa na mipango ya Yanga.
Mpira uligeuka kutumika kwa mabavu hasa upande wa JKT Tanzania wakionekana kutumia nguvu zaidi kwa Yanga.
JKT walifanya mabadiliko mengine dakika 72 wakimtoa Edward Songo na kuingia Mohamed Rashid kwenda kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji wakati huo huo Yanga walimtoa Sibomana na kuingia Mrisho Ngassa.
Mabadiliko ya Mo Rashid yalionyesha kitu safu ya ushambuliaji kwa JKT  baada ya kucheza sambamba na Adam Adam.
Dakika ya 86, Yanga ilikosa bao la nne baada ya Ngassa kumtoka beki wa JKT, Frank Nchimbi na kupiga pasi kwa Balinya lakini umakini wa kipa Abdulrahman Mohamed aliucheza mpira huo.

Advertisement