Molinga apiga mbili Yanga ikiichapa Friends Rangers

Muktasari:

Mchezo huo wa kirafiki ni wa kwanza kwa Yanga tangu kusimama kwa Ligi Kuu Bara kupisha mechi za Kimataifa katika kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Dar es Salaam. Mshambuliaji David Molinga amefunga mabao mawili akiingoza Yanga kushinda 4-3 dhidi ya Friends Rangers katika mchezo wa kirafiki kwa kujipima nguvu uliochezwa kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam.

Mshambuliaji Molinga alifunga mabao mawili huku magoli mengine yakifungwa na Maybin Kalengo pamoja Papy Kabamba Tshishimbi.

Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Kalengo kabla ya Molinga kufunga mara mbili akitanguliwa kufunga bao la kwanza kwa njia ya mkwaju wa adhabu ndogo.

Bao hilo la mpira wa adhabu Molinga ni kama anarudia ambapo amewahi kufunga bao kama hilo wakati Yanga ikipata sare ya mabao 3-3 na Polisi katika mechi ya Ligi Kuu.

Bao la tatu kwa Yanga limefungwa na mshambuliaji Tshishimbi kwa shuti kali huku Molinga akikaribia kufunga Hat Trick baada ya kukosa mkwaju wa penalti iliyogonga mwamba na kutoka nje na kuifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele mabao 4-0.

Kipindi cha pili kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila alifanya mabadiliko kadhaa akiwatoa wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza na kuwaingiza wa wachezaji wa kikosi cha vijana na kuwafanya Rangers kuzinduka.

Kipindi hicho Rangers ikicheza soka ka kuelewana walifanikiwa kupata bao la kwanza likifungwa kwa shuti kali  na Laurent Peter aliyenufaika na makosa ya mabeki wa Yanga kuzembea  kukosa mpira wa adhabu ndogo kabla ya Robert Mwakila kufunga bao la pili huku Abeid Kisiga akifunga la tatu na kufanya mchezo huo kumalizika kwa Yanga kushinda kwa mabao 4-3.

Kocha Mwandila alisema mchezo huo hakuwa na lengo la kuangalia ushindi ambapo wamepata nafasi ya kuangalia kipimo cha wachezaji wao waliokosa kucheza mechi mbalimbali sambamba na kupima kipimo cha mazoezi yao tangu kusimama kwa ligi.