Molinga awasapraizi Yanga Dar

HUKU ikielezwa kwamba Kocha Luc Eymael amewaambia viongozi hatamuongezea mkataba, David Ndama Molinga ‘Falcao’ yeye ana ishu yake ambayo akiwaambia viongozi itakuwa sapraizi kubwa kwao.

Mchezaji huyo ambaye ametulia zake ghetto Jijini Dar es Salaam, ameliambia Mwanaspoti kwamba mkataba wake na Yanga unamalizika mwezi Agosti ila atawapa kipaumbele kabla ya kusaini dili nyingine kwavile ameishi nao muda mrefu tena kwa uzuri.

Molinga alisema amepata ofa kutoka Etoile Sportive Du Sahel inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Tunisia ambayo inamtaka akafanye majaribio ya siku 15 pamoja na Sidi Kacem ya Daraja la Pili siku 10.

“Nimepokea tena barua ambayo ninayo hapa kwangu ndani kutoka katika timu ya Union Sidi Kacem, kutokea Ligi Daraja la Pili nchini Morocco ambayo nayo imenitaka nikafanye mazoezi na wachezaji wao kwa pamoja kwa muda wa siku kumi kisha baada ya hapo ndio mazungumzo na wao ya kunisainisha mkataba yataanza,” alisema.

“Timu nyingine zaidi ya tatu zipo nyumbani kwetu DR Congo zinashiriki Ligi Kuu pamoja na mashindano ya kimataifa ambazo zote zinanitaka nikasaini mkataba moja kwa moja lakini nao nimewajibu wasubiri nitawapa majibu hapo nitakapomaliza mkataba wangu na Yanga Agosti.

“Kabla ya kufanya uamuzi wangu wowote nitawafuata viongozi na kuwaonesha barua na ofa ambazo nimezipata kutoka katika timu nyingine kama watataka kunibakisha nitawasikiliza maslahi yao lakini kama ikiwa tofauti na hivyo ndio nitafanya uamuzi wangu,

“Etoile na Union Sidi Kacem zote zilikuwa zinanitaka niende huko kwao tena kipindi kabla ya janga hili la corona kutokea lakini nimeshindwa kusafiri kwanza lazima niwaonyeshe viongozi barua zangu hizo za kuhitajika huko na wao wanipe ruhusa,” alisema Molinga.