Moura wa Spurs aitwa Brazil

Muktasari:

  • Kocha wa timu ya Taifa ya Brazil, Tite amemuita mshambuliaji wa Tottenhm, Lucas Moura katika kikosi chake kitakachocheza mechi mbili za kirafiki nchini Saudi Arabia dhidi ya wenyeji mchezo utakaopigwa Ijumaa hii wakati mchezo mwingine utachezwa siku nne baadaye dhidi ya Argentina.

London, England. Mshambuliaji wa timu ya Tottenham Hotspur ya Ligi Kuu ya England, Lucas Moura, ameitwa kwenye kikosi cha Brazil kwa mara ya kwanza baada ya kutoitwa kwa miaka miwili.

Mchezaji huyo aliyeonyesha kiwango cha hali ya juu kwenye kikosi cha Spurs msimu huu jambo lililomshawishi Kocha Adenor Leonardo Bacchi maarufu kama Tite kumjumuisha kwenye kikosi chake kinachojiandaa kwa mechi mbili za kirafiki.

Brazil itajitupa uwanjani keshokutwa mjini Riyadh kukipiga na wenyeji wao Saudi Arabia na siku nne baadaye kusafiri hadi mji wa Jeddah ambako itacheza na mahasimu wao Argentina.

Mratibu wa michezo ya timu ya Taifa ya Brazil, Edu Gaspar alizitangaza mechi hizo jana Jumatatu mjini Rio de Janeiro kuwa mechi hizo ni muhimu kwa ajili ya kujiweka fiti.

Moura, mwenye miaka 26, ameitwa kuchukua nafasi ya winga wa Everton, Gremio ambaye ni majeruhi wa nyama za paja.

Gaspar amebainisha kuwa gharama za mechi hizo zote zinabebwa na Serikali ya Saudi Arabia ambayo ndiyo iliyoomba mechi hizo ili kuipa mazoezi timu yao ya Taifa.