Mpira umewavunjia ndoa wachezaji hawa

Wednesday April 1 2020

 

By Olipa Assa

MPIRA ni starehe kwa mashabiki na wadau wengine, lakini vilevile ni ajira kubwa duniani kwani vijana wengi wameajiriwa kupitia soka na wanalipwa mamilioni ya fedha.

Lakini wakati mwingine usipouangalia vizuri unaweza kukuletea shida. Mwanaspoti limefanya mahojiano na baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu Bara ambao wameeleza namna umbali ulivyovunja mahusiano na wengine ndoa zao, kisa soka kuwafanya wawe na muda mfupi wa kukaa na wenza wao.

RAMADHAN CHOMBO ‘REDONDO’

Unamkumbuka huyu jamaa alivyokichafuaga Simba enzi zile. Alikuwa si mchezo pale dimba la kati. Sasa hivi ni kiungo wa Biashara United.

Jina lake halisi ni Ramadhan Chombo ‘Redondo’. Ni kati ya wachezaji ambao ndoa zao zilivunjika kutokana na muda mfupi aliokuwa anapatikana nyumbani.

Wakati anasimulia kisa hicho hakutaka kutaja jina la mtalaka wake, lakini anasema walikuwa na miaka mitano ya uchumba na baada ya kuona amekolea kimapenzi wakafunga ndoa mwaka 2012.

Advertisement

“Nilifunga ndoa 2012, tuliachana mwaka 2016 tukiwa tumezaa mtoto mmoja anaitwa Ashfat wa kike ana miaka 11, namlea mwenyewe,” anasema.

Anasema sababu kubwa anaamini kuwa huenda yeye hakuwa mtu sahihi kwa mama mtoto wake na pia mwanamke hakupangiwa na Mungu.

“Aliendelea na maisha mengine, kapata mtu sahihi kwake si unajua kazi zetu, kuhusu kuoa nasubiri kwanza nisije nikamtesa mtoto wa watu hapo baadaye, nikitulia kwa maana ya kuzunguka basi nitatafuta ubavu wangu ingawa sio kila mwanamke mvumilivu,” anasema.

MOHAMED SAMATTA

Kiungo wa KMC, Mohamed Samatta anasema wakati anacheza Mgambo JKT ya Tanga, mchumba wake ambaye amezaa naye mtoto wa kiume alimsaliti na kwenda kuendelea na maisha mengine.

Anasimulia kwamba alishaanza kuambiwa na marafiki zake kwamba mchumba wake alikuwa na njia tofauti kisha akapata ushahidi, na kama haitoshi akamthibitishia kwamba ni kweli.

“Alinishangaza sana, nikagundua ni umbali wa kazi zangu, mbaya zaidi yeye kanithibitishia, maumivu makali yalinichukua siku tatu, wakati wa mazoezi nilikuwa natingwa hivyo sikuwaza sana, nikikaa mwenyewe najikunja kitandani na kusema kwa nini,” anasema.

“Sikutajii jina hata hivyo, kukuambia nimekuheshimu sana, nilishamsahau kwa sasa nina mke ninayempenda anaitwa Nuru Ramadhan ambaye anajua nawajibika kwa ajili yake.”

MARCEL  KAHEZA

Mshambuliaji wa Polisi Tanzania, ambaye anamiliki mabao saba na pasi tano za mabao umbali umemfanya aachane na mchumba wake ambaye wamedumu miaka mitatu.

Ana-sema kisa mchumba wake alikuwa anataka ukaribu muda wote na kwamba alishindwa kuivumilia kazi yake.

“Nimeachana naye miezi mitatu iliyopita, uchumba wetu ni miaka mitatu, shida yake alikuwa haelewi kuhusu majukumu yangu, nikaamua kila mtu ashike hamsini zake,” anasema Kaheza.

“Sijaumizwa na hilo labda yeye, kwani naamini nitapata binti mwingine mimi mwanaume, afanye yake nafanya yangu,” anasema.

JOSEPH KIMWAGA

Mshambualiji wa Biashara United, Joseph Kimwaga ni miongoni mwa wachezaji ambao walijikuta wanapoteza mahusiano kisa umbali wa kuwa na mchumba wake.

Anasema msimu wa 2013/14 Azam FC walichukua ubingwa wa Uhai Cup na alikuwa nyota kwenye michuano hiyo, hilo lilifanya aonekane na kila mtu.

Anasema alikuwa na rafiki yake ambaye alikuwa na mdogo wake wa kike mrembo, akamwambia msichana huyo anampenda.

“Kipindi hicho nilikuwa mtu wa dini, rafiki yangu aliponiambia mdogo wake ananipenda nikaheshimu hisia zake, hapo ndipo nilipoanzia mahusiano.

“Akanipenda kupita kiasi lakini wakati huo nguvu zangu nilizielekeza kucheza sana, yeye alitaka muda mwingi niwe naye, sikutilia manani nisingeacha kusafiri na timu kwani ndio kazi ilikuwa inanipatia ugali,” anasema.

“Nakumbuka mwisho wa mapenzi yetu ulikuwa wakati nipo na Simba akaamua kuendelea na maisha yake, sikumlaumu na sijamchukia namuombea apate furaha ya mapenzi huko aliko,” anasema. Maisha ndio hayo tena, kumbe mastaa wetu kwenye soka nao wana mambo mazito.

Advertisement