Mshindi wa Mchongo wa Mwanaspoti anogewa aitaka bodaboda

Muktasari:

  • Mshindi wa shindano la ‘mchongo wa Mwanaspoti’ wa zawadi ya Sh100, 000, Ursula Mohamed amesema fedha hizo atazitumia kuongeza mtaji wake wa genge.

Morogoro. Mshindi wa shindano la mchango wa Mwanaspoti Ursula Mohamed mkazi wa kihonda maghorofani manispaa ya Morogoro amekabidhiwa kitita chake cha Sh. 100,000 na kuahidi fedha hizo kuzitumia kwa kuongeza mtaji wake wa genge.

Ursula mwenye umri wa miaka 60, alisema ushindi huo umempa chachu ya kucheza shindano hilo kwani anaamini ipo siku atafanikiwa kupata bodaboda ama simu ya mkononi kupitia shindano hilo ambalo litaendeshwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Julai 1 mwaka huu.

Alisema yeye ni mpenzi wa michezo hivyo katika matumizi yake ya kila siku amekuwa akitenga bajeti ya kununua gazeti la Mwanaspoti ili kupata habari za michezo hususani mpira wa miguu.

“Hata kabla ya shindano hili mimi ni mpenzi wa gazeti la mwanaspoti kama sina hela nipo tayari nikope hela ili ninunue gazeti la mwanaspoti,” alisema Ursula.

Meneja mauzo wa kampuni ya Mwananchi mkoa wa Morogoro, Aziz Msuya alisema amefarijika mkoa wa Morogoro kutoa mshindi wa shindano hilo kwani kwa kiasi kikubwa ushindi huo utaongeza hamasa kwa wananchi kununua na kusoma gazeti la Mwanaspoti.

Akieleza namna ya kucheza shindano hilo Msuya alisema kuwa mshiriki anatakiwa kununua nakala ya gazeti hilo la Mwanaspoti na kujaza kuponi iliyoko kwenye gazeti hilo na baadaye kuipeleka kwenye ofisi za gazeti hilo.