Msola ampa mbinu Aussems

Muktasari:

  • Dk Msola alitaja maeneo ambayo Aussems anapaswa kufanyia kazi ni safu ya ulinzi, kiungo, ushambuliaji na kutumia mbinu ya kupata ushindi ugenini.

Dar es Salaam. Wakati droo ya mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikitarajiwa kufanyika leo nchini Misri, Kocha wa Simba Patrick Aussems ametakiwa kurekebisha mambo makubwa manne katika kikosi chake.

Simba inatarajiwa kuanza mechi zake mbili za robo fainali kwa kuvaana na Esparance ya Tunisia, TP Mazembe ya DR Congo au Wydad Casablanca ya Morocco.

Pamoja na rekodi nzuri za Simba katika mechi za nyumbani za kimataifa, aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Dk Mshindo Msola amemtaka Aussems kuchukua tahadhari kutokana na ugumu wa wapinzani wao.

Rekodi nzuri katika mechi za nyumbani ilizonazo Esparance, TP Mazembe na Wydad Casablanca, zinaiweka Simba katika nafasi ngumu ya kushinda ugenini dhidi ya vigogo hivyo.

Katika mechi nne ilizocheza Simba ilishinda zote dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland, Nkana ya Zambia, Al Ahly ya Misri na AS Vita ya DR Congo.

Mabingwa watetezi Esperance katika mechi sita ilishinda tatu nyumbani, ilitoka sare mbili na kupoteza mchezo moja ugenini, TP Mazembe katika mechi nane ilishinda nne nyumbani, ilitoka sare tatu na kupoteza mchezo mmoja ugenini.

Wydad Casablanca katika mechi nane ilishinda tatu, ilitoka sare moja nyumbani na kupoteza mechi tatu ugenini na kushinda moja.

Baadhi ya wadau akiwemo Dk Msola alisema timu hiyo ina nafasi ya kufanya vyema katika mashindano hayo endapo Aussems atafanyia kazi mambo manne.

Dk Msola alitaja maeneo ambayo Aussems anapaswa kufanyia kazi ni safu ya ulinzi, kiungo, ushambuliaji na kutumia mbinu ya kupata ushindi ugenini.

Alisema mabeki wamekuwa wakifanya makosa yaleyale tangu kuanza mechi za mashindano jambo ambalo ni hatari watakapovaana na wapinzani wao katika robo fainali.

“Ni jukumu la mabeki kutafakari wanakosea wapi kabla benchi la ufundi kuwasaidia. Safu ya ulinzi imekuwa ikirudia makosa, hakuna maelewano,” alisema Dk Msola.

Pia alisema Aussems anatakiwa kufanyia kazi eneo la kiungo mshambuliaji na alimtaja Haruna Niyonzima ni mchezaji wa kuigwa kutokana na aina ya mchezo aliocheza dhidi ya AS Vita.

“Lazima benchi la ufundi na wachezaji wahakikikishe wanatatua tatizo la kufungwa mechi za ugenini ili lisijirudie. Bahati ya kushinda nyumbani inaweza isiwepo tena, wajipange kushinda ugenini,” aliongeza Dk Msola.

Alisema wachezaji wanapaswa kuandaliwa kisaikolojia mapema kwamba wana uwezo wa kushinda hata mechi za ugenini au kutoka sare.

Kocha wa Prisons, Mohammed ‘Adolph’ Rishard alisema safu ya ushambuliaji inapaswa kupewa makali kabla ya kuanza mechi za robo fainali.

“Ukiangalia mchezo uliopita dhidi ya Vita Simba ilicheza vizuri hasa dakika 30 za mwisho, kile kiwango walistahili kushinda na kuonyesha kuwa kweli wanaweza kucheza mashindano haya.

Rishard alisema endapo Aussems ataongeza mbinu katika safu ya ushambuliaji, ana matumaini Simba itapata matokeo mazuri katika mechi zake.

Hata hivyo, Rishard kama ilivyokuwa kwa Dk Msola alisema safu ya ulinzi inapaswa kucheza kwa tahadhari hasa mabeki Zana Coulibaly na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliodai wamekuwa wakipanda mbele, lakini wanashindwa kurejea kwa wakati katika nafasi zao