Msolla ukweli ni huu kisa jezi ya 'Simba'

WAKATI Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla akivunja ukimya kuhusu tuhuma kwamba yeye ni ‘mnyama’, imefahamika uongozi wa klabu hiyo umeshitakiwa na nyota wake wakishinikiza kulipwa fedha za malimbiko wanayodai kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania (Sputanza), Mussa Kissoky amethibitisha kupokea malalamiko ya wachezaji wanne wa Yanga wanaoidai klabu hiyo na kusisitiza suala lao kwa sasa limehamishiwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa uamuzi zaidi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kissoky aliwataja wachezaji walioamua kuushtaki uongozi wa miamba hiyo ya Jangwani ni Andrew Vincent ‘Dante’, Pato Ngonyani, Haji Mwinyi Mngwali na Matheo Anthony waliowasilisha malalamiko yao kwao.

“Ni kweli wachezaji hao wamekuja na wameeleza madai yao, sisi tunaendelea na taratibu za kuhakikisha wanapata stahiki zao kwa kufuata utaratibu,” alisema Kissoky.

Aidha, ameeleza mpaka sasa hatua ambayo wamechukua ni kumwandikia barua Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao ambapo nakala ya barua hiyo pia imetumwa kwa klabu ya Yanga ili ijibu madai hayo.

Kisoky alisema kwa sasa ni Kidao na wenzake kulifikisha jambo hilo mbele ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji, kwaajili ya kujadiliwa kwa kuhusisha pande zote mbili.

Pato anayekipiga kwa sasa Polisi Tanzania alithibitisha kupeleka malalamiko hayo kwa vile Yanga imeshindwa kumsikiliza kumlipa malimbikizo ya fedha za usajili na malimbikizo ya mshahara.

“Yanga naidai fedha nyingi zaidi ya Sh 10 milioni ambazo ni za usajili na malimbikizo ya mishahara ya miezi zaidi ya mitatu, kitu ambacho tangu nimeanza kufuatilia sijapewa,” alisema Pato huku, Mwinyi naye akikiri kufanya hivyo kwa madai kuwa lengo ni kuona haki yake inafanyiwa kazi na kupewa stahiki zake.

“Nawadai fedha nyingi sana Yanga sina sababu ya kuweka wazi ni kiasi gani, kikubwa mkataba wangu unajieleza hivyo ni siri yangu mimi na mwajiri wangu kikubwa ninachoweza kukwambia ninawadai,” alisema.

MSOLLA HUYU HAPA

Dk Mshindo alipoulizwa juu ya taarifa hizo za kuburuzwa TFF kwa kushindwa kuwalipa haki zao wachezaji hao waliotimka klabu hapo, alisema ni ngumu kulijibu kama limefika TFF, lakini alidai Yanga ya sasa ni tofauti na ile ya nyuma.

“Tuliingia madarakani tulikuta wachezaji wanasotea mishahara, lakini leo hii kucheleweshewa siku mbili, imekuwa nongwa kwa watu ambao wanatafuta pa kutokea.

“Ndani ya muda mfupi tulitengeneza mazingira ya mishahara kwa wachezaji wetu, isitoshe kila wiki tunawapa posho laki moja kila mtu, ila kwa kuwa kuna genge la watu ambao ni asilimia 10 Yanga limeamua kuropoka wanafanya hivyo,” alisema.

Alisema hayo yanayotokea sasa aliyatarajia na si mageni kwake ila anafarijika kuona asilimia 90 ya Wanayanga wanaunga mkono uongozi wao na asilimia 10 ndiyo wanavuruga.

APANGUA TUHUMA

Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na tetesi kwamba Dk Msolla anajiandaa kujiuzulu kwa vile anatuhumiwa kuwa Simba damu, lakini mwenyewe amemua kuvunja ukimya akisema amesikia kupitia mitandano ya kijamii , lakini ni kundi la watu wasioitakia mema Yanga.

“Nimeona watu wananihusisha kuwa upande wa Simba, kisa nilivaa jezi ya rangi ya Simba,” alisema Dk Msolla alipokuwa akizungumza na gazeti hili.

Alisema kuna kundi la watu limeamua kumchafua kwa kuwa tangu wameingia madarakani wameziba mianya ya kupiga pesa za klabu kwa watu hao waliokuwa wakifanya miaka ya nyuma.

Kuhusu kuwa ameandika barua na kabla ya Desemba ataachia ngazi, Dk Msolla alisema sio kweli, ila imevumishwa na watu aliowaita wapigaji waliozoea kuitumia Yanga kujinufaisha.

“Sijaandika barua, huo ni uvumi wa baadhi ya watu ambao baada ya kuzibiwa mianya ya upigaji wameanza kutapatapa na kuibua maneno ambayo hayana ukweli,” alisema na kuongeza;

“Shida watu walizoea mfumo wa zamani, sasa tumetengeneza mfumo ambao utajenga taasisi imara Yanga wanaanza fitina ili mambo yasiende kwa kuwa wanakosa fursa za kujinufaisha binafsi.”

“Baada ya kuona maslahi yao yamezibwa, ndiyo wameamua kuanzisha fitina ambazo hazina kichwa wala miguu, wengine wametafuta picha ya miaka mingi nimevaa jezi ya rangi nyekundu ili mradi kutengeneza mgogoro.”

Alisema picha hiyo ni ya muda mrefu akiwa timu ya Moro Veterans ambapo yeye ndiye muasisi.

“Moro Veterani inavaa jezi ya rangi yoyote, mwaka jana mimi nimewapelekea jezi za njano, wanavaa, zipo za bluu, kijani na nyinginezo, timu haina rangi, wanayoletewa na wadau wake wanavaa,” alisema.

Akizungumzia kuhusika kwake kwenye usaili wa Kocha wa Simba, Patrick Aussems, Dk Msolla alisema watu wenye akili watajua kipi ni kipi kwenye hilo ikizingatiwa kuwa yeye kitaaluma ni kocha.