Msuva ataka vijana U17 kupambana

Muktasari:

  • Msuva alisema fursa waliyonayo vijana hao mbali na kuiletea heshima taifa ni kujitangaza wao wenyewe ili waweze kupata nafasi za kujiunga na klabu kubwa barani Ulaya.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Difaa El Jadida ya Morocco, Saimon Msuva amesema wachezaji wa timu ya vijana ya Tanzania yenye umri chini ya miaka 17 ’Serengeti Boys’ wanatakiwa kutumia vema fursa ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana (Afcon) ili kupata nafasi ya kucheza Ulaya.

Msuva mwenye mabao 10 aliyofunga msimu huu kwenye Ligi Kuu Morocco alisema atafuatilia kwa karibu Fainali hizo zinazoanza leo hadi Aprili 28 huku Serengeti Boys ikifungua dimba kwa kucheza na Nigeria.

Msuva alisema fursa waliyonayo vijana hao mbali na kuiletea heshima taifa ni kujitangaza wao wenyewe ili waweze kupata nafasi za kujiunga na klabu kubwa barani Ulaya.

“Wenzetu wa Afrika Magharibi sio ajabu kuna wachezaji wao wengi wanatoka kwenye timu kubwa za vijana Ulaya, tunawezaje na sisi kuwa na wachezaji wetu huko ni kwa kutumia hii fursa. “Mpira wa sasa ni vijana nimeshuhudia huku Morocco, wanamkazo kwenye soka la vijana, watafuta vipaji vingi kutoka sehemu mbalimbali na naamini watakuwa Tanzania kusaka vipaji vingine.

“Uwepo wao huko ni ngumu kumuacha mchezaji ambaye atawavutia, Tanzania tuna vipaji na kuchelewa kwetu kutoka ndiko kulikotukwamisha kutambuika,“ alisema.