Mtanzania aingia anga za Pacquiao

Tuesday September 11 2018

 

By Imani Makongoro, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mtanzania Hassan Mwakinyo ameweka rekodi nyingine ya dunia kwa kuingia katika orodha ya kuwa bondia namba 16 kwa viwango vya ubora duniani.

Mwakinyo ameweka rekodi muda mfupi baada ya kumdunda kwa TKO bondia wa Uingereza Sam Eggington katika pambano la uzito wa super welter.

Mafanikio ya bondia huyo yamemuingiza katika anga za mabondia maarufu duniani Athony Joshua wa Uingereza na Manny Pacquiao anayetokea Philippines.

Hii ni mara ya kwanza kwa bondia wa Tanzania kupata mafanikio makubwa katika medani ya ngumi duniani.

Mwakinyo ambaye ni mkazi wa mkoani Tanga, ameishangaza dunia baada ya kumchakaza mpinzani wake katika pambano lililokuwa la utangulizi baina ya Amir Khan dhidi ya Samuel Vargas.

Baada ya ushindi huo, Mwakinyo ameingia kwenye rekodi akiwa bondia pekee wa Afrika aliyeingia kwenye orodha ya mabondia 50 bora wa dunia katika uzito wa super welter.

Ushindi wa ‘Technical Knock Out’ (TKO) wa raundi ya pili dhidi ya mpinzani wake anayeshika nafasi ya nane kwa ubora duniani umeitangaza vyema Tanzania katika mchezo wa masumbwi.

Wakati Mwakinyo akipanda, mpinzani wake ameporomoka hadi nafasi ya 30 kwa viwango vya ubora duniani.

Mwakinyo amepata nyota nne na nusu katika ubora wa ngumi na anakaribia kuingia katika rekodi ya bondia namba moja wa dunia kwenye uzito huo Jarett Hurd raia wa Marekani ambaye ana nyota tano.

Idadi hiyo ni sawa na ile ya nguli wa uzito wa juu duniani raia wa Uingereza Joshua na Pacquiao ambao pia wana nyota tano kila mmoja.

Rekodi ya Mwakinyo iliyoacha mshituko Uingereza imempa fursa ya kuandaliwa pambano la kuwania ubingwa wa Kimataifa wa IBF kwa vijana litakalopigwa Oktoba 20 Ujerumani dhidi ya Wanik Awdijan.

Kauli ya Serikali

Pamoja na Mwakinyo kusisitiza kuendeleza rekodi aliyoiweka Uingereza kwenye pambano la Ujerumani, Serikali inamuandalia mapokezi makubwa atakaporejea nchini.

Akizungumza kwa simu jana Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema Serikali itamsaidia katika mkakati wake wa kujiandaa na mapambano mengine.

“Atakapofika nchini tutakaa naye kujua tunamsaidia vipi katika pambano lake la Ujerumani, lazima tumsaidie, sasa hivi atakuwa akiangaliwa na mabondia wakubwa zaidi lakini ili afike mbali, lazima twende kimkakati.

“Tujipange tumsaidie aweze kuendeleza rekodi zaidi ili kuwa bingwa mkubwa wa dunia na kuipa heshima nchi na yeye kunufaika kwa kipaji chake,” alisema Waziri Mwakyembe.

Dk Mwakyembe alisema Mwakinyo ni matunda ya Serikali kuingilia kati kumaliza vurugu zilizokuwepo muda mrefu kwenye ngumi za kulipwa.

Wadau wafunguka

Mbali na kauli ya Serikali, kocha wa zamani wa timu ya Taifa, Nassor Michael alisema Mwakinyo ana nafasi ya kuwa bondia bora duniani kama Joshua endapo atapata msingi mzuri kuanzia sasa.

“Kinachohitajika ni maandalizi, anapaswa kuwa na kocha mwenye kiwango bora, ikiwezekana atakaporejea nchini kutoka Uingereza aanze kambi mapema kujiandaa na pambano la Oktoba,” alisema Michael aliyewahi kuwa kocha wa timu ya Taifa iliyofuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008.

Michael alimtaka bondia huyo kuongeza uzito wa ngumi anazorusha kwa sababu kwa kuwa atakutana na mabondia hodari duniani.

Bondia Amos Mwamakula alisema kuwa Mwakinyo anahitaji kuungwa mkono na Serikali wakati akijiandaa na pambano jingine la Ujerumani.

“Mwakinyo sasa sio bondia wa ‘uswahilini’ amekuwa staa, kitendo cha kumpiga Muingereza tena bondia namba nane wa dunia sio jambo dogo, hiyo ni nembo yetu kwenye ngumi,” alisema Mwamakula.

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa (BFT), Chris Mutta alisema Mwakinyo anatakiwa kupata kocha bora atakayempa mbinu za kiufundi.

“Alicheza vizuri nilichokiona alicheza kwa kasi sana kama angekutana na bondia anayemudu hadi raundi ya saba, kwa kasi aliyoanza nayo kuna uwezekano naye angechoka. Nashauri afanye mazoezi makali ya pumzi kujiandaa na pambano la Ujerumani,” alisema.

Advertisement