Mtanzania aisogelea rekodi ya Hasheem NBA

Dar es Salaam. Mchezaji chipukizi wa Tanzania, Atiki Ally amesema kuchaguliwa kwake kwenye timu ya kwanza ya wachezaji nyota wa vyuo nchini Canada kumemunyooshea ndoto ya kucheza Ligi ya Kikapu nchini Marekani (NBA).

Atiki aliyepo nchini Canada kwa sasa akitokea Chuo cha Themes Valley District School Board, anafuata nyayo za mchezaji wa kwanza Mtanzania kusajiliwa NBA, Hasheem Thabeet anayeichezea Fort Wayne Mad Ants iliyopo Indiana nchini Marekani.

“Kwa kweli nimefurahi sana na sikutegemea kama ningechaguliwa kwenye timu ya kwanza kutokana na uwezo mkubwa wa wachezaji wenzangu walioonyesha kwa kila mchezo,” alisema Ally ambaye hata hivyo bado hajajua kama atasajiliwa na timu kubwa au la katika siku za karibuni.

Kwa kawaida wachezaji wanaofuzu katika hatua hiyo hujiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kuchaguliwa na timu zinazoshiriki Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), ambayo inasifika kwa kulipa fedha nyingi wachezaji wake.

Akielezea siri ya uteuzi wake, Ally alisema ilitokana na kujituma muda wote uwanjani  pamoja na kuhakikisha anaipatia ushindi timu yake.

Hata hivyo, hakusita kumpongeza kocha wake Mtanzania Bahati Mgunda aliyempa moyo na kumtaka asikate tamaa huku akimsihi kuwa msikivu kwa kufuata maelekezo anayopewa na makocha.

Ally amechaguliwa kwenye timu ya kwanza ya wachezaji nyota na National Preparatory Association (NPA) chini Canada, na taarifa kutoka nchini humo zimeeleza kuwa kuchaguliwa kwake kunatokana na uwezo mkubwa aliouonyesha kwa kila mchezo aliocheza.

Mchezaji huyo alipata udhamini wa kusoma katika Chuo cha Themes Valley District School Board nchini humo baada kuonyesha kiwango kizuri katika mafunzo yaliyokuwa yanaendeshwa na mkufunzi wa timu ya taifa, Matthew McAllister kutoka Marekani mwaka 2017.

Makocha wanasemaje?

Bahati Mgunda, kocha wa timu ya Taifa ya vijana ya kikapu chini ya miaka 18 anasema anafurahia maendeleo mazuri ya Ally katika mafunzo yake nchini Canada, pamoja na kucheza kwa kiwango cha juu katika mashindano.

“Ninachoweza kusema ni kwamba Ally anafanya vizuri sana, tunachohitaji ni kumuombea ili aendelee kupaa juu,” alisema Mgunda

Naye Isiaka Juma, kocha wa Temeke alimtaka Ally asibweteke  kwa kuteuliwa kwenye timu ya kwanza ya wachezaji nyota nchini Canada, kwani bado safari ni ndefu.

“Nachomuomba aongeze jitihada zaidi katika mafunzo anayopewa na makocha wake nchini Canada,” alisema kocha huyo.

Kocha wa timu ya Vijana, Kabiola Shomari alisema kuteuliwa kwa Ally kumeonyesha njia kwa vijana wengine wanaojifunza mchezo wa kikapu.

Ally alianza kucheza kikapu mkoani Mwanza, kisha alijiunga na Shule ya Msingi ya Gerezani, Dar es Salaam na baada ya kumaliza elimu ya msingi alijiunga na Sekondari ya High View huku akichezea timu ya Vijana.

Alikopita Hasheem

Hasheem kwa upande wake alipita Sekondari ya Makongo kabla ya kuibukia Marekani alikojiunga na programu ya mafunzo ya mchezo wa kikapu katika Chuo Kikuu cha Connecticut (UCCON) kati ya 2006–2009, kabla ya kuchaguliwa katika mchujo wa kwanza wa wahitimu wa mafunzo hayo uliofanyika 2009 ambapo alidondokea katika timu ya Memphis Grizzlies.

Kwa sasa mchezaji huyo anaichezea Fort Wayne Mad Ants inayoshiriki Ligi G ya NBA yenye maskani yake katika mji Fort Wayne uliopo Indiana nchini humo.

Mbali na timu hizo, mchezaji huyo amewahi kuzichezea timu za Houston Rockets, Rio Grande Valley Vipers, Portland Trail Blazers, Oklahoma City Thunder, Grand Rapids Drive, Los Angeles Lakers zote za Marekani pamoja na Yokohama B-Corsairs ya Japan.