Mtanzania atua mikononi mwa Mayweather

Muktasari:

  • Mwakinyo amekuwa gumzo kila pembe ya dunia, baada ya kuushangaza ulimwengu wa masumbwi aliposhinda pambano lake kwa ‘Technical Knock Out’ (TKO) ya raundi ya pili dhidi ya mpinzani wake aliyekuwa akishika nafasi ya nane kwa viwango vya ubora duniani kabla ya kuporomoka hadi nafasi ya 30.

Dar es Salaam. Mambo yanazidi kumnyookea bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo baada ya kunyemelewa na idadi kubwa ya mawakala na mapromota mbalimbali duniani kufuatia ushindi wake wa kishindo dhidi ya nyota wa Uingereza Sam Eggington.

Mwakinyo amekuwa gumzo kila pembe ya dunia, baada ya kuushangaza ulimwengu wa masumbwi aliposhinda pambano lake kwa ‘Technical Knock Out’ (TKO) ya raundi ya pili dhidi ya mpinzani wake aliyekuwa akishika nafasi ya nane kwa viwango vya ubora duniani kabla ya kuporomoka hadi nafasi ya 30.

Bondia huyo aliyejiandaa kwa wiki mbili kwa pambano hilo, ananyemelewa na kampuni maarufu ya bondia nyota duniani, Floyd Mayweather inayoitwa ‘The Money Team’ (TMT).

Mayweather ana rekodi ya aina yake katika ngumi akiwa amecheza mapambano 50 na kushinda yote yakiwemo 27 aliyoshinda kwa ‘Knock Out’ (KO).

Akizungumza kwa simu jana, bondia huyo alisema amebaki Uingereza kwa muda na atarejea nchini wiki hii.

Mwakinyo mwenye miaka 23, alisema kwa takribani miaka miwili iliyopita alikuwa ndoto ya kuwa bondia bora wa ngumi za kulipwa, lakini hakutarajia kufikia kiwango cha kuishangaza dunia.

“Mimi ni bondia mchanga na masikini sana, lakini leo (jana) nimepokea ofa kutoka kwa mapromota, watafutaji wa mapambano ya ngumi na watu ambao wanataka niwe chini yao.

“Kilichonishitua zaidi ni kuitwa na Kampuni ya TMT ambayo inamilikiwa na bondia Floyd Mayweather, nimeshangaa sana. Dakika 15 tu zimeniwezesha kuwashangaza wadau wa ngumi za kulipwa duniani,” alisema Mwakinyo.

Bondia huyo alisema muda mfupi baada ya kumalizika pambano hilo, alifuatwa na watu mbalimbali wakiwemo mapromota na mawakala waliotaka kujua historia yake ya ngumi, nchi anayotoka na mawasiliano ya kumpata.

“Namshukuru Rashid Nassor na aliyenitafutia pambano Coffie Azumah ambaye alifanya kazi kubwa kuwaelewesha wadau wa ngumi za kulipwa, hii imenipa mwanga mkubwa katika fani yangu ambayo nimekumbana na vikwazo vingi mpaka kufikia hapa,” alisema Mwakinyo.

Alisema mafanikio aliyopata ni makubwa, hivyo anatakiwa kutuliza akili kuchagua kambi nzuri ya kujiunga nayo nje ya nchi baada ya kupata ushauri wa kiufundi. Mwakinyo alisema licha ya kupata ofa kutoka kambi ya Mayweather, lakini atatafakari akisubiri kupata muongozo mzuri kabla ya kutia saini mkataba na kampuni sahihi.

“Kama nilivyosema natoka familia masikini ambayo hata uwezo wa kununua gunia la mazoezi haina, natumia tairi la gari kufanyia mazoezi, tena siyo kwenye ‘gym’ katika uchochoro wa mtaani, nahitaji kupata muongozo sahihi ili kuepuka stori za mabondia nyota wa zamani ambao kwa sasa wanaishi maisha tofauti.

“Suala la Mayweather na wengine hilo linahitaji umakini mkubwa, nitahusisha Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) na wadau wengine ili kuona nafikia wapi, hii ni nafasi yangu ya kudhihirisha dunia kuwa Tanzania ina mabondia hodari,” alisema Mwakinyo.

Historia

Mwakinyo alizaliwa mkoani Tanga katika eneo la Makorora ambapo kabla ya kucheza ngumi alianzia ‘kickboxing’ akifuata nyayo za kaka yake Hamisi Mwakinyo.

Mwaka 2015 aliamua kujikita katika ngumi baada ya kupata ushindi kwa kutumia mikono badala ya mateke ambayo pia yanatumika katika mchezo wa ‘kickboxing’.

“Sikuona sababu ya kuendelea na kickboxing kwa sababu mateke hayakunipa ushindi zaidi ya kutumia mikono, nikajua kipaji changu kipo kwenye ngumi na moja kwa moja nilianza ngumi za kulipwa,” alisema Mwakinyo.

Alisema ameishi maisha magumu kwa kuwa alipata fedha ndogo za kununua mahitaji yake ya kila siku kupitia ngumi za mtaani.

Safari Uingereza

Awali, Mwakinyo hakuwemo katika mpango wa kwenda kuzichapa katika pambano hilo kabla ya neema kumshukia kufuatia bondia kutoka Ghana kujiengua zikiwa zimebaki wiki mbili.

Mwakinyo alipata fursa hiyo baada ya mshirika wa promota, Juma Ndambile anayemiliki Kampuni ya Don Chief Promotion, Coffie Azumah kuanza kusaka bondia wa kujaza nafasi ya Mghana.

Alisema alipata nafasi baada ya mtoto wa Azumah kuona ‘clip’ yake kwenye mitandao akifanya mazoezi kwa kutumia tairi la gari na muda mfupi baadaye alipewa taarifa ya kutakiwa kwenda Uingereza kucheza pambano la utangulizi.

“Mimi sina kocha maalumu kaka yangu Hamisi, Rashid na rafiki yangu Bella Puza ndiyo walikuwa wakinipa moyo kuwa nitashinda pambano hilo kwa mazoezi ambayo nilikuwa ninafanya,” alisema Mwakinyo.

Matumla ampa somo

Mshindi wa medali ya shaba katika uzito wa feather kwenye michezo ya Madola mwaka 1994, Hassan Matumla amemtaka Mwakinyo kuwa makini baada ya kupata mafanikio kimataifa.

“Alipofikia Mwakinyo anapaswa kuwa na kocha mzuri wa kumuendeleza, asiwape nafasi mapromota ‘uchwara’ wa bongo ambao wengi ni wajanja, atulie na apige hesabu ya mapambano makubwa sio tena ya uswahilini,” alisema Matumla.

Nahodha wa zamani timu ya Taifa ya ngumi za ridhaa, Mzonge Hassan amemtaka bondia huyo kutobweteka baada ya kupata umaarufu.

“Nimemfahamu Mwakinyo tangu tukiwa majirani Tanga hadi alipojiunga na ngumi za ridhaa kabla ya kucheza za kulipwa ni bondia ambaye hakati tamaa anajua nini anahitaji,” alisema Mzonge.

Kocha maarufu wa ngumi nchini, Habibu Kinyogoli alisema bondia huyo anatakiwa kuishi maisha ya kuzingatia nidhamu kwa kufuata masharti ya ngumi ndani na nje ya ulingo.