Mtendaji Simba aanika mambo mazito Msimbazi

Dar es Salaam. Wakati mtendaji mkuu mpya wa Simba, Senzo Mazingisa akitimiza miezi mitatu na siku nane ofisini, ametaja mambo ambayo anataka kuyafanya ndani ya klabu hiyo.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu baada ya kutembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) jijini hapa jana, Mazingisa alisema kuna mambo mengi ambayo anataka kuyafanya na baada ya muda mfupi klabu hiyo itakuwa na ofisi maalumu.

Mtendaji huyo ambaye alianza kazi Septemba 7 akichukua nafasi ya Crescentius Magori, alisema hivi karibuni klabu hiyo itakuwa na ofisi za kisasa zitakazoendeshwa kwa kuzingatia weledi.

“Sote tunajua kwamba tuna zile ofisi za Msimbazi, zipo kwa miaka mingi, sasa zimekuwa na changamoto kutokana na kuingiliana na wanachama. Nataka kuwahakikishia kwamba tutakuwa na ofisi ya kisasa itakayoongozwa na muundo mzuri wa kiuongozi, nafikiri mpaka sasa ni kama asilimia 90 zimekamilika,” alisema.

“Hii itakuwa ni yetu kama Simba, mwenyekiti wetu wa bodi (Mohamed Dewji ‘MO’) ametupatia, lakini nina furaha kwamba baada ya wiki chache tutakuwa ndani ya ofisi ambazo zitakuwa zimekamilika kila kitu kwa kila ofisi itakayokuwa hapo, ambazo zitaifanya Simba kutoka ilipo na kwenda mbali zaidi.”

Senzo alisema ofisi zilizopo katika jengo la mtaa wa Msimbazi zitakarabatiwa na kuendesha mambo ya wanachama, huku zile zitakazokuwa kwenye jengo la Diamond Plaza lililopo katikati ya jiji zikiwa maalumu kwa mambo ya kiutendaji.

Mtendaji huyo ambaye aliambatana na mjumbe wa bodi ya klabu hiyo, Mulamu Ng’ambi, alisema tayari ameikabidhi bodi ya Simba uhalisia wa hesabu za uendeshaji wa vikosi vyote vya timu pamoja na zile za kiuendeshaji.

Alisema katika taarifa hiyo bodi imeona ni jinsi gani gharama za uendeshaji zimekuwa kubwa kuliko fedha zinazoingia katika klabu hiyo ambapo kwa sasa mpango endelevu ni kuhakikisha Simba inatumia vyanzo vya mapato ilivyo navyo ili kuongeza fedha.

“Ripoti hii imeanzia katika kikosi cha timu ya vijana, timu kubwa na mpaka timu ya wanawake, vitu vyote tunavyokodi, malipo ya makocha, wachezaji na kiasi cha fedha tunachotumia kulipa wafanyakazi posho,” alisema.

“Bodi imepata picha halisi ya gharama, iliwashtua lakini hivi ni vitu ambavyo tulihitaji kuvijua na baada ya hapo sasa ni lazima tusumbue akili jinsi gani tutapunguzaje gharama za uendeshaji.”

Alisema hivi karibuni alikutana na mmoja wa wanachama aliyelalamikia timu kutoweka kambi, suala ambalo alilipinga.

“Niliposikia hilo Ijumaa ya wiki iliyopita nikawaambia wasaidizi wangu watoe picha ya wapi tuliingia mkataba wa miaka mitano kwa ajili ya kambi ambayo wachezaji wanaitumia,” alisema.

“Unajua sio kazi yangu kama mtendaji kushinikiza kwamba timu ikae kambini, inategemea na maamuzi ya benchi la ufundi, sisi wengine kazi yetu ni kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa na kumpa (kocha) ushirikiano wa kutosha.”

Mtendaji huyo alisema miongoni mwa makosa makubwa wanayofanya watawala ni kuonyesha wanajua ukocha.

“Haipo hivyo, kazi yetu kubwa ni kutengeneza mazingira mazuri kwa makocha na wachezaji kufanya kazi zao,” alisema.

Senzo aliongeza kuwa kwa sasa wako katika mchakato wa kuhakikisha wanapitia leja ya idadi ya wanachama walio hai ikiwa ni njia ya kuanza kuwatumia kwa maendeleo ya klabu.