Mtibwa yaiporomosha Yanga

Sunday January 14 2018

 

By Oliver Albert, Mwananchi [email protected]

Mtibwa Sugar imeiporomosha Yanga hadi nafasi ya tano baada ya kuichapa Lipuli kwa bao 1-0, mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Ushindi huo umeifanya Mtibwa Sugar kufikisha pointi 24 na wakati Yanga ikiwa ya tano na pointi 21, huku Singida United ikiwa ya nne kwa pointi 23 kabla ya mechi yake dhidi ya vinara Simba (26) na Azam yenye pointi 26.

Hata hivyo, msimamo huo wa ligi utanoga zaidi baada ya mechi za Alhamisi. Jumatano ijayo, Yanga itacheza na Mwadui na siku inayofuata, Simba itaikaribisha Singida United kwenye Uwanja wa Uhuru.

Siku hiyo, Azam nayo itakuwa mjini Songea kuifuata Majimaji.

Mechi za jana

Mtibwa Sugar ilipata bao lake dakika ya 34, lililofungwa na Hassan Dilunga kwa shuti la karibu kwa mguu wa kushoto.

Kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, wenyeji Ndanda FC walishindwa kutumia vizuri uwanja wao baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbao.

Mbao iliyoifunga Yanga mabao 2-0 mwishoni mwa mwaka jana, ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Emmanuel Mvuyekule kabla ya Ndanda kusawazisha kupitia kwa Nassor Kapama.

Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga, ‘Chama la Wana’ Stand United wameendeleza ubabe wao dhidi ya Ruvu Shooting kwa kuichapa kwa bao 1-0.

Ligi hiyo itaendelea leo kwa mchezo mmoja mkoani Mbeya kwa Prisons kuwakabili Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine.

Katika michezo ya Ligi ya Daraja la Kwanza, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa Sh 2milioni kuwazawadia Coastal Union baada ya kuishinda 3-0 Kurugenzi Mufindi.

Mabao ya Coastal yalifungwa na Andrew Simchimba, Omary Salum na Raizan Hafidi.

Matokeo mengine, JKT Tanzania iliilaza Mvuvumwa mabao 3-0 huku Mgambo ikiitandika Kiluvya 3-1.

Rhino Rangers iliifanyizia Dodoma FC kwa kuilaza mabao 2-0, sawa na Biashara iliyoifunga Alliance. Mlale JKT ikaibandua 1-0 Mawenzi sawa na Mshikamano ilivyoifunga Ashanti United. Toto na JKT Oljoro hakuna mbabe, zikatika suluhu.

Advertisement