Stars, mdogo, mdogo

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ jana ilivuna pointi moja kwenye mchezo wa kusaka nafasi ya kufuzu fainali za Afrika hapo mwakani, ilipoilazimisha Uganda ‘The Cranes’ kutoka nayo suluhu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Kampala.

 

BY Thomas Ngi’tu, Mwananchi

IN SUMMARY

  • Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Kocha mpya wa Taifa Stars, Emmanule Amunike nyota wa zamani wa Nigeria ‘Super Eales’ ambaye hivi karibuni alisaini mkataba wa miaka miwili kuinoa Stars.

Advertisement

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ jana ilivuna pointi moja kwenye mchezo wa kusaka nafasi ya kufuzu fainali za Afrika hapo mwakani, ilipoilazimisha Uganda ‘The Cranes’ kutoka nayo suluhu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Kampala.

Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Kocha mpya wa Taifa Stars, Emmanule Amunike nyota wa zamani wa Nigeria ‘Super Eales’ ambaye hivi karibuni alisaini mkataba wa miaka miwili kuinoa Stars.

Bila shaka kwake huu ni mwanzo mzuri wa kuanza na pointi ugenini tena mbele ya timu ambayo ipo juu kwa mujibu wa viwango vya ubvora wa Fifa.

Hata hivyo, mchezo wa jana ulitibuliwa na mvua kubwa iliyonyesha uwanjani hapo kabla ya kuanza kwa mchezo huo, na kusababisha utelezi kuwanyima vijana wa Stars kuonyesha umahiri.

Wenyeji Uganda waliokuwa wakishangilia kwa nguvu kwa matarajio kuwa wangejipatia ushindi kirahisi, walikutana na kazi pevu uwanjani hadi kuwalazimisha kunyamaza kadiri muda ulivyosonga.

Uganda walimtegemea zaidi Emmanuel Okwi anayekipiga Simba SC kupata mabao kwa kuwa anawajua vema walinzi wa Taifa Stars, lakini mambo hayakuwa rahisi kwake kama alivyodhani kwani hadi mapumziko timu zilikuwa hazijafungana.

Safu ya ulinzi ya Stars, iliyokuwa chini ya kipa, Aishi Manula, Hassan Kessy, Abdi Banda, Aggrey Morris na David Mwantika ilijitahidi kucheza kwa umakini na kuhakikisha haimpi mwanya Okwi kupata bao.

Baada ya Uganda kufanya mashambulizi matatu ambayo hayakuwa na madhara Stars ilijibu katika dakika ya 14 pale winga mwenye kasi Saimon Msuva alipowachomoka walinzi lakini akashindwa kutumia nafasi aliyoipata kwa kupiga shuti jepesi lililodakwa na kipa wa Uganda, Denis Onyango.

Nafasi pekee nzuri waliyoipata Uganda ni ile ya dakika ya 22, pale Okwi alipofanikiwa kuingia na mpira ndani ya 18 lakini alishindwa kufanya lolote akiwa na mpira miguuni na mabeki wa Stars kuuondosha.

Dakika 24 Uganda walipata faulo iliyopigwa na Godfrey Walusimbi, lakini umahiri wa Aishi Manula ulisaidia kwani aliupangua mpira huo na kuwa kona tasa.Dakika 26 Stars Mbwana Samatta alichezewa faulo na Nicholas Wadada aliyeonyshwa kadi ya njano hata hivyo shuti la Msuva, lilitoka sentimeta chache.

Dakika 40 Joseph Benson alikosa goli la wazi baada ya kuiwahi krosi na Okwi, huku mabeki wa Stars wakidhani mchezaji huyo ameotea, hata hivyo papara zake zikamfanya ashindwe kuipatia bao la kuongoza.

Katika safu ya ushambuliaji ya Stars ilionekana kutokuwa na maelewanao huku kikosi kikicheza kwa kujilinda zaidi, kwani Thomas Ulimwengu alikuwa akicheza peke yake huku Samatta na Msuva wakicheza kwa nyuma.

Kutokana na uwanja kuteleza kipindi cha kwanza licha ya kuwepo kwa mashambulizi machache kutokana na timu kulazimika kufanya mashambulizi ya kuviziana lakini pia timu zililazimishwa kubutua badala ya kugonga pasi za chini, hivyo kwenda mapumziko zikiwa 0-0.

Mfumo wa 3-4-3 uliokuwa unatumiwa na Stars katika mchezo huo haukuwa na tija sana katika kujenga mashambulizi ya uhakika, ingawa katika kujilinda yalisaidia lakini yaliifanya Stars kushambulia mara chache hasa ikizingatiwa kuwa utelezi ulimzuia Msuva kufanya vitu vya kwa mbinu walizopanga kuzitumia.

Katika kipindi cha pili timu zote ziliamua kutumia mipira ya juu katika kupeleka mashambulizi, huku ufundi wa kuchezea mpira kwa vijana wa Stars ukizidi kupoteza kutoka na mazingira ywa uwanja yalivyokuwa.

Katika dakika ya tatu ya kipindi cha pili, Gadie Michael alipiga shuti kali lakini likapanguliwa na kipa wa Uganda na kuwa kona ambayo haikuleta manufaa yoyote kwa Stars.

Dakika 56 Msuva alifanyiwa madhambi, lakini faulo iliyopigwa na Samatta, ilitoka nje kidogo ya lango, jambo lililomfanya Kocha wa Uganda kufanya mabadiliko kwa kumtoa Joseph Ochaya na kumuingiza Patrick Kaddu.

Dakika 70 Samatta aliikosesha Stars bao baada ya kuwatoka walinzi wa Uganda na kumchambua kipa Onyango, lakini hesabu zake zilikataa kwani alipojaribu kuurejesha mpira nyuma kwa kuchopu ili afunge ukamgonga kipa huyo na akaudaka.

Kocha Amunike naye alifanya mabadiliko kwa kumtoa Gadiel Michael na kuingia Farid Mussa, lengo likiwa ni kuongeza kasi ya mashambulizi lakini naye hakuleta shangwe iliyosubiriwa.

Dakika 74 Msuva alimiliki mpira vizuri na kupiga krosi ndani ya lango la Uganda na kukutana na Thomas Ulimwengu, lakini naye hesabu zake hazikuwa sahihi kwani shuti lake lilipanguliwa na kuwa kona tasa.

Katika dakika 78 Amunike alimpumzisha Frank Domayo na kuingia Himid Mao, akilenga kuimarisha safu ya kiungo ambayo ilianza kutaliwa na Uganda ambayo nayo ilimtoa Emmanuel Okwi na kuingia Luwaga Kizito.

Matokeo hayo yanaifanya Uganda kuendelea kukalia kiti cha Kundi L ikiwa na pointi nne wakati Stars imepaa hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi mbili baada ya mechi mbili.

Mechi nyingine ya kundi hilo inafanyika leo wakati Lesotho itakapokabiliana na Cape Verde.

Cape Verde ilifungwa na Uganda 2-1 mchezo wa kwanza wakati Lesotho ilitoka sare ya 1-1 na Tanzania.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept