Mwakinyo: Wanaosema nimebebwa hawajui ngumi

Dar es Salaam. Hassan Mwakinyo amewajibu mashabiki wanaoponda ushindi wake wakidai amebebwa na majaji.

Mwakinyo aliibuka mshindi kwa pointi dhidi ya Arnel Tinampay wa Ufilipino Ijumaa iliyopita jijini Dar es Salaam.

Jaji namba moja alitoa ushindi wa pointi 97-93 na jaji namba mbili alitoa pointi 98-92 kwa Mwakinyo huku jaji namba tatu akitoa sare ya pointi 96-96.

Ushindi huo uliibua mjadala kwa mashabiki wa ndondi nchini ambao baadhi walidai Mwakinyo ‘amebebwa’ na majaji na hakustahili kushinda kwa namna walivyolitazama pambano hilo.

“Huo ni mtazamo wao, siwezi kuwapinga wala kuwazuia wasizungumze, binafsi sina utaalamu wa urefarii au ujaji kwenye ngumi,” alisema Mwakinyo akifafanua ushindi huo.

“Ni kweli lilikuwa pambano gumu, lakini mpinzani wangu alinipiga ngumi nyingi za mbavu kwa lengo la kunichosha na kunikata pumzi ili atafute matokeo ya KO (knock out) jambo ambalo hakufanikiwa kwani nilifanya mazoezi ya kutosha ya pumzi,” alisema.

Bondia huyo namba moja Afrika kwenye uzani wa super welter alilifananisha pambano lake na Tinampay na lile la Floyd Mayweather na Manny Pacquiao.

“Wengi walibeza ushindi wa Mayweather wakiamini amebebwa na majaji lakini ndiye alipiga ngumi nyingi za pointi kulinganisha na Pacquiao ambaye kweli alirusha ngumi nyingi zaidi, lakini asilimia kubwa ziliishia kifuani na tumboni kwa Maywether ambazo hazikuwa za pointi.

Ashiriki mazishi ya mashabiki wake

Jana Jumapili bondia huyo aliungana na waombolezaji wengine katika mazishi ya mashabiki waliotoka Tanga kwenda Dar es Salaam kushuhudia pambano hilo.

Mashabiki hao walipoteza maisha katika ajali iliyohusisha basi la Coastal Union na lori walipokuwa njiani kurudi Tanga baada ya pambano hilo.

“Tunawaombea majeruhi wengine wapone haraka, lakini wenzetu wawili waliopoteza maisha mmoja tayari tumempumzisha katika nyumba yake ya milele na mwingine atazikwa leo (jana) saa saba mchana,” alisema.

Waliopoteza maisha walitajwa kuwa kuwa ni Barack Obama na Ibrahim Omary.