Mwakinyo apanda viwango vya dunia

Muktasari:

  • Mwakinyo sasa ana rekodi ya kucheza mapambano 18, ameshinda mapambano 16 (11 kwa KO) amepigwa mara mbili (moja kwa KO.

Dar es Salaam.Siku chache baada ya kumchapa Arnel Tinampay wa Ufilipino kwa pointi, bondia Hassan Mwakinyo amepanda kwa nafasi mbili kwenye viwango vya ngumi vya Dunia katika uzani wa super welter.
Katika viwango hivyo vinavyotolewa na mtandao wa ngumi wa dunia (Boxrec), Mwakinyo amepanda hadi nafasi ya 17 kutoka nafasi ya 19 aliyokuwa awali.
Mtanzania huyo mwenye nyota nne kati ya tano ambazo ni za kiwango cha juu na cha mwisho katika ngumi za kulipwa licha ya kupanda hadi nafasi ya 17 duniani, ameendelea kuwa namba moja Afrika kwenye uzani wake.
Katika viwango hivyo, Mwakinyo amefikisha pointi 156.5 huku  Jaime Munguia  wa Mexico akikamata namba moja akiwa na pointi 546.7 na nyota tano.
Erislandy Lara amekuwa wa pili kwa kupata pointi 482.4 na Julian Williams amehitimisha tatu bora ya dunia kwenye uzani huo kwa kupata pointi 481.9, wote raia wa Marekani.
Aliyewa bondia namba moja katika uzani huo, Jarrett Hurd ameporomoka hadi nafasi ya nne akiwa na pointi 412.5.
Katika viwango vya Afrika, Mwakinyo ameendelea kung'ang'ania namba moja akiwapiku Mnigeria Wale Omotoso ambaye anashika nafasi ya pili na Mohammed Rabii wa Morocco  aliyekamata nafasi ya tatu.
Watanzania wengine, Twaha Kiduku na Maono Ally wameingia  kumi bora  katika viwango vya Afrika kwenye uzani wa super welter ambapo Twaha  yuko nafasi ya  saba na Maono wa tisa.