Mwakinyo awapa raha Watanzania kuelekea mechi ya Stars v Uganda

Muktasari:

 

  • Pambano hilo ni la tatu mfululizo kwa Mwakinyo kushinda kwa TKO tangu alipoweka rekodi ya kumchapa Sam Eggington nchini Uingereza mwisho mwa mwaka jana kwa TKO, kisha Said Yazidu na Joseph Sinkala.

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo ameendeleza ubabe baada ya kuchapa Sergio Eduardo Gonzalez kwa Technical Knock Out (TKO) raundi ya tano ya pambano lililokuwa la raundi nane.

Mwakinyo ndani ya dakika tatu za raundi ya tano alimtandika mpinzani wake ngumi 12 mfululizo bila majibu.

Gonzalez alilazimika 'ku gurd' muda wote kabla ya kujikuta akienda chini kana kwamba anapiga magoti, lakini hakuweza kustahimili makonde ya Mwakinyo na kwenda moja kwa moja chini.

Bondia huyo Muargentina hakumudu kuendelea na pambano hilo hilo na kulazimika kusalimu amri kwa Mwakinyo kwa kuruhusu kipigo cha TKO.

Hata kabla ya pambano hilo, Mwakinyo alionekana yuko fiti tangu anapanda ulingoni saa 4:6 Usiku akiwa ameambatana na wasaidizi wake (Seconds).

Huku bendera za Tanzania zikipepea ndani ya Ulingo kwenye ukumbi wa mikutano wa Kenyatta mara baada ya Mwakinyo kupanda ulingoni, alizunguka pande zote kuwasabahai mashabiki ambao walikuwa wakimshangilia.

Baada ya kengere ya kuashiria kuanza kwa raundi ya kwanza ya pambano hilo la uzani wa super welter, Mwakinyo alianzisha mashambulizi na mpinzani wake akijibu, lakini kadri dakika zilivyosogea, Gonzalez alionekana kuchoka na kushindwa kuhimili kasi ya Mwakinyo.

Mtanzania mwingine, Iddi Mkwera, alimchapa Mkenya Nicholas Mwangi kwa TKO katika pambano la utangulizi la kumsindikiza Fatuma Zarika na Catherine Phiri wa Malawi la kuwania ubingwa wa dunia wa WBC kwa wanawake.