Mwakinyo azidi kuporomoka viwango vya ngumi duniani

Muktasari:

  • Rekodi zinaonyesha Hassan Mwakinyo, amepanda ulingoni mara 18 na kushinda mapamban0 16, huku 11 yakiwa ya KO na kupoteza mawili likiwamo moja la KO na hajawahi kupata sare tangu ajipoingia kwenye ngumi hizo za kulipwa mwaka 2015.

WAKATI janga la ugonjwa wa corona ukizidi kukwamisha wanamichezo kupata fursa ya kupambana, Bondia Mtanzania Hassan Mwakinyo amezidi kuporomoka kwenye viwango vya ubora wa ngumi vya dunia (boxrec).
Bondia huyo namba moja nchini kwenye uzani wa Super Welter ameporomoka hadi nafasi ya 86 kutoka ile ya 24 aliyokuwa anaishikiri katika orodha hiyo ya ubora wa ngumi duniani.
Mwakinyo aliyewahi kupanda hadi kufikia nafasi ya 16 duniani kwenye uzani huo mara baada ya kumchapa Sam Eggington, amezidi kupata wakati mgumu wakati huo hakuwa na mwenendo mzuri katika viwango hivyo.
Licha ya kushinda mapambano yake manne baada ya lile la Eggington, Mtanzania huyo alishuka hadi nafasi ya 19 kabla ya kushuka tena wiki mbili zilizopita hadi nafasi ya 24 na sasa ameporomoka zaidi hadi nafasi ya 86.
Mbali na kuporomoka, Mwakinyo amepoteza nyota moja na nusu kati ya nne alizokuwa nazo awali na hii imekuja wakati pambano lake dhidi ya Mjerumani Jack Culcay, lililokuwea lichezwe Machi 21 likiahirishwa kwa sababu ya tishio la ugonjwa wa corona.
Pambano hilo lilikuwa la kuwania ubingwa wa kimataifa wa WBO, ubingwa mkubwa baada ya ule unaoshikiliwa na Manny Pacquiao.