Mwakyembe aagiza bondia aliyedundwa Ulaya afungiwe

Wednesday June 19 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk Harrison Mwakyembe ameagiza bondia Selemani Bangaiza aliyepigwa kwa Technical Knock Out (TKO) Jumamosi iliyopita nchini Australia afungiwe.

Waziri Mwakyembe alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya video ya pambano hilo kumuonyesha Bangaiza akisalimu amri kwa mpinzani wake bila kupigwa ngumi.

Video hiyo ilionyesha Bangaiza amesimama kwenye kona yake wakati mpinzani wake, Andrew Moloney akijiandaa kurusha ngumi.

Mtanzania huyo alinyoosha mkono juu kuonyesha ishara ya kutoendelea na pambano kabla ya kutema kilinda ulimi (mouth guard) ulingoni. Baada ya ishara hiyo, mwamuzi alimaliza pambano huku Moloney akimpongeza Bangaiza ambaye alikubali kipigo cha TKO raundi ya kwanza.

Mwakyembe alisema ingawa mchezo una matokeo ya kushinda na kushindwa, lakini si kwa namna ilivyotokea kwa Bangaiza.

“Mambo kama haya yanarudisha nyuma michezo nchini, huyu bondia lazima afungiwe ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema waziri huyo.

Advertisement

Kocha aliyeambatana na bondia huyo, Anthony Rutha alisema hajui sababu za Bangaiza kusalimu amri kwa kuwa hakupigwa ngumi ambayo ilimchanganya na kushindwa kuendelea.

“Nimemuuliza sababu za kuachia pambano hanipi majibu ya kueleweka, Bangaiza ni kama amefanya ujanja maana ameacha pambano kiajabu ajabu,” alisema Rutha.

Akizungumzia tukio hilo, bondia huyo alidai hajafanya hujuma kwa kuwa mkakati wake ulikuwa ni kupata ushindi dhidi ya mpinzani wake.

“Sijui nini kilitokea, lakini nilihisi maluweluwe nikiwa ulingoni,” alisema Bangaiza. 

Advertisement