Mwamuzi Sasii kuchezesha Simba, Sevilla Dar es Salaam

Monday May 20 2019

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania mwenye beji ya Fifa, Hery Sasii amepangwa kuchezesha mchezo wa kirafiki kati ya Simba na Sevilla itakayochezwa Alhamisi, Mei 23 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa mashindano wa TFF, Salum Madadi alisema uamuzi wa kumteua Sasii umetokana na mwamuzi huyo kufuzu vigezo vilivyowekwa kuelekea mchezo huo.

"Kama mnavyofahamu uteuzi wa marefa unafanyika kwa taratibu zilizowekwa na baada ya kamati zetu kukaa na kujadiliana, mwamuzi tuliyemteua kuchezesha mechi hiyo ni Hery Sasii na mwamuzi msaidizi namba moja atakuwa ni Mohammed Mkono na msaidizi namba tatu atakuwa ni Soud Lila.

“Katika kuonyesha kuwa tunawathamini na kutambua mchango wa akina mama, mwamuzi namba nne atakuwa ni Jonesia Rukyaa," alisema Madadi.

Madadi alisema ujio wa Sevilla una maana kubwa kwa soka la Tanzania na shirikisho hivyo watahakikisha wanautumia vyema fursa ya kuleta maendeleo ya soka la Tanzania.

"Tunawapongeza SportPesa kwa mchango wao kwa mpira wa miguu Tanzania. Wamekuwa wakizileta timu mbalimbali kutoka nje ya nchi jambo ambalo lina faida kubwa kwenye soka letu.

Advertisement

Ujio wa timu hii umetuunganisha vizuri zaidi na La Liga (Ligi Kuu ya Hispania) na kuuimarisha zaidi uhusiano wetu na sisi kama shirikisho tunaona hii ni nafasi nzuri kwetu kunufaika nao," alisena Madadi.

Advertisement