Mwanamke kuchezesha kwa mara ya kwanza Ligue 1 Ufaransa

Muktasari:

  • Uamuzi wa kumpangia mechi ya mwishoni mwa wiki umetokana na ombi la Fifa kutaka waamuzi walioteuliwa kuchezesha fainali za Kombe la Dunia la wanawake wapewe mazingira mazuri na bora ya maandalizi.

Kwa mara ya kwanza wikiiendi hii, Ligi Kuu ya soka ya wanaume nchini Ufaransa, itachezeshwa na refa mwanamke, Stephanie Frappart atakapopuliza filimbi katioka mechi baina ya Amiens na Strasbourg, Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) limetangaza.
Frappart, 35, anapiga hatua kubwa zaidi baada ya kuchezesha mechi za Ligue 2, ambayo ni ya pili kwa ukubwa, tangu mwaka 2014.
Pia atakuwa mwamuzi wakati wa fainali za Kombe la Dunia za wanawake zitakazofanyika Ufaransa mwezi Juni na Julai.
FFF ilisema uteuzi wa refa wa mechi hiyo ya Jumapili unatokana na ombi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kusaidia waamuzi watakaochezesha fainali za Kombe la Dunia kujiandaa katika mazingira bora kwa ajili ya michuano hiyo.
Mwamuzi wa Ujerumani, Bibiana Steinhaus alikuwa refa wa kwanza wa kike katika ligi kubwa barani Ulaya baada ya kuchezesha mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, baina ya Hertha Berlin na Werder Bremen mwezi Septemba, 2017.