Tanesco haikamatiki mashindano Shimuta yaichapa Sua

Muktasari:

Mashindano hayo yanafanyika jijini Mwanza yakishirikisha timu 16 katika michezo mbalimbali ikiwamo soka, wavu, kikapu na kuvuta kamba.

Mwanza. Timu za tano za Tanesco zimeendelea kung’ara kwa kufanikiwa kutinga katika hatua ya robo na nusu fainali katika mashindano ya Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Kampuni Binafsi za Tanzania (Shimuta) yanayoendelea Jijini Mwanza.

Michuano hiyo inafanyika jijini Mwanza kwa mara ya kwanza, inashirikisha timu 16 katika michezo mbalimbali ikiwamo soka, wavu, kikapu na kuvuta kamba.

Katika mchezo wa soka uliopigwa leo Disemba 5 kwenye Uwanja wa Nyamagana, Tanesco ikicheza kwa kujiamini ilifanikiwa kutoa kichapo kwa SUA cha mabao 4-0 na kutinga katika hatua ya robo fainali.

Mabao ya Tanesco yalifungwa na Adam Said na Kurwa Mangara kila mmoja akifunga mabao mawili katika mechi hiyo iliyokuwa ya upande moja.

Nyota ya Tanesco iliendelea kung’ara katika mchezo wa mpira wa pete baada ya kuichakaza Mloganzila kwa magoli 63-18 na kufanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali.

Katika mpira wa wavu wanawake Tanesco iliduwaza UDSM kwa seti 3-0 katika robo fainali na kufanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Tanesco iliendeleza ubora wake katika mpira wa wavu kwa wanaume baada ya kuifunga MOCU kwa seti 3-0 na kufuzu kwa nusu fainali.

Katika mpira wa kikapu Tanasco imefanikiwa kutinga nusu fainali ya mashindano hayo baada ya kuifunga IFM kwa pointi 51- 23 katika robo fainali iliyokuwa na ushindani mkali.

Awali timu ya IFM imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Shimmuta baada ya kuitandika TPDC kwa penalti 4-1 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.