Mwenyekiti Kamati Uchaguzi TFF ajiuzulu

Muktasari:

  • Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Revocatus Kuuli, ameandika barua ya kujiuzulu kwa madai  ya kuingiliwa majukumu ya kiutendaji na baadhi ya viongozi wa shirikisho hilo.

 

Dar es Salaam. Hatimaye Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shrikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Revocatus Kuuli amejiuzulu wadhifa wake.

Hivi karibuni Wakili Kuuli alitishia kujizulu nafasi ya mwenyekiti kwa madai ya kamati yake kuingiliwa na kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza kwa simu, Wakili Kuuli ametaja sababu ya kuachia ngazi ni kamati yake kuingiliwa majukumu yao ya kiutendaji na baadhi ya vigogo ndani ya TFF.

Alisema amekuwa akisimamia sheria, lakini amekumbana na vikwazo kutoka kwa baadhi ya vigogo ndani ya shirikisho hilo waliokuwa na dhamira ya kumkwamisha.

Makamu wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani kujiuzulu Wakili Kuuli hakuwezi kuathiri shughuli za kiutendaji kwa  kuwa kamati yake inaendelea na kazi.

Wakili Kuuli ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo wakati uchaguzi  mkuu wa Simba ukitarajiwa kufanyika Novemba 3, mwaka huu.

Mchakato wa uchaguzi wa Simba umefikia hatua ya wagombea kukata rufani baada ya kupitia mapingamizi.

Pia Bodi ya Ligi inatarajiwa kufanya uchaguzi mdogo kuziba nafasi ya mwenyekiti iliyoachwa wazi na Clement Sanga aliyejiuzulu.

Septemba 17, Wakili Revocatus Kuuli alitangaza kusimamisha mchakato wa uchaguzi wa Simba kutokana na kile alichokisema kutofuatwa baadhi ya utaratibu na kanuni za uchaguzi.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye Katibu Mkuu wa TFF Wilfried Kidao alidaiwa kumuandikia barua Wakili Kuuli kueleza sababu za kusitisha uchaguzi wa Simba.