Mwenyekiti Lipuli, Matola kila mtu kivyake

Muktasari:

  • Matola ameinoa Lipuli kwa mafanikio na kuiwezesha kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) na kufungwa bao 1-0 na Azam iliyotwaa ubingwa.

Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa klabu ya Lipuli, Benedict Kihwelu akisisitiza bado klabu hiyo inamtambua Suleiman Matola kuwa kocha wao, kocha huyo amekanusha akidai kwa sasa hana mkataba wa klabu hiyo ya Iringa.

Matola nyota na nahodha wa zamani wa Simba alisema hana mkataba wa kuendelea kuinoa timu hiyo kauli ambayo imepingwa vikali na mwenyekiti huyo wa Lipuli aliyedai kocha huyo bado ni mali yao.

"Matola ni kocha wetu na bado tuna mkataba naye, kama anasema hana mkataba na sisi hayo ni maneno yake tu, lakini ninachokifahamu kama mwenyekiti kocha huyo bado ni muajiliwa wa Lipuli," alisisitiza.

Bosi huyo wa Lipuli alisema, klabu yao haijafikiria kuachana na Matola na ndiye kocha ambaye wataendelea kuwa naye kwa msimu ujao.

Hata hivyo Matola amekanusha vikali akisisitiza hana mkataba na klabu hiyo na si kocha wa Lipuli kwa sasa.

"Hata nilipokuwa naifundisha sikuwa na mkataba, sikusaini kwa kuwa kuna vitu havikuwa sawa, hivyo nilikuwa nafundisha kwa makubaliano ya mdomo tu, lakini hawakunipa mkataba," alisema Matola.

Alisema hivi sasa ni kocha huru kwani hana mkataba na timu yoyote na hata Lipuli ambao wanasema ni kocha wao hawajazungumza naye chochote baada ya Ligi kumalizika.

"Makubaliano yaliyokuwepo ni kufundisha mpaka mwishoni mwa msimu, lakini sikusaini mkataba," alisisitiza Matola.