Mwisho wa enzi! Yondani akili inataka mwili unagoma

Muktasari:

Yondani ni miongoni mwa wachezaji wenye bahati ya kupata idadi kubwa ya mataji nchini na kwa kiasi kikubwa mchango wake umehusika katika hilo.

Dar es Salaam. Baada ya kutamba katika soka la Tanzania kwa takribani miaka 13, ni wazi kwamba zama za nyota wa Yanga na timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, Kelvin Yondani zinaelekea ukingoni.

Uamuzi wa benchi la ufundi la Yanga kumuanzisha benchi beki huyo mwenye umri wa miaka 36 katika mchezo wa mechi ya watani wa jadi dhidi ya Simba uliochezwa, Machi 8 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam inaweza kuwa ishara ya hitimisho la enzi kwa beki Yondani mzaliwa wa jijini Mwanza.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa pil Yanga ilishinda bao 1-0 lililofungwa na nyota wa kigeni Bernard Morrison. Mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabaom 2-2.

Kuwekwa nje Yondani ambaye aliingia uwanjani dakika za lala salama za mechi hiyo kulikuwa ni mwendelezo wa benchi la ufundi la Yanga chini ya kocha Luc Eymael ambaye ameonekana hajakoshwa na kiwango cha libero huyo.

Eymael amekuwa akipendelea kumtumia zaidi beki Said Juma ‘Makapu’ kucheza nafasi ya beki wa kati sawa na Lamine Moro huku Yondani akijikuta akisotea benchi na wakati mwingine kutazama mechi akiwa jukwaani.

Pamoja na kusota benchi, bado beki huyo aliyezaliwa mwaka 1984 ameendelea kuwa tegemeo la timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na ametajwa miongoni mwa wachezaji walioitwa kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).

Hata hivyo, fainali hizo pamoja na zile za Chan zimesitishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Inawezekana Yondani akafanikiwa kurudisha namba yake ndani ya kikosi cha Yanga lakini kwa umri alionao na changamoto ya kuibuka kwa kundi kubwa la vijana wanaocheza vyema safu ya ulinzi, ni jambo lililo wazi miaka michache ijayo, Yondani anaweza kutundika daluga ili kutoa nafasi kwa wengine.

Ikiwa Yondani ataachana na soka anabaki kuwa mmoja wa wachezaji walioutendea haki mchezo wa soka kutokana na kile alichofanya kwa muda wote anaocheza soka la ushindani.

 

Kung’ara Simba na Yanga

Si rahisi mchezaji kuzitumikia klabu mbili kongwe na kubwa nchini za Simba na Yanga na akapata mafanikio na kuheshimika lakini hilo ni tofauti kwa Yondani ambaye ameweza kufanya hivyo.

Beki huyo amecheza kwa mafanikio katika timu hizo zote mbili ambazo amezitumikia kwa nyakati tofauti akianzia Simba aliyojiunga nayo mwaka 2007 na baada ya kucheza kwa miaka mitano akatimkia Yanga alikocheza miaka minane.

Katika miaka 13 ambayo amezitumikia timu hizo, amefanikiwa kuwa katika kikosi cha kwanza na tegemeo la safu za ulinzi za timu zote mbili.

 

Rafiki wa Mataji

Yondani ni miongoni mwa wachezaji wenye bahati ya kupata idadi kubwa ya mataji nchini na kwa kiasi kikubwa mchango wake umehusika katika hilo.

Ametwaa mataji takribani 13 katika ngazi ya klabu na timu ya Taifa na bila shaka kwa kizazi hiki ndiye mchezaji aliyefanikiwa kunyanyua idadi kubwa ya mataji kuliko wengine.

Katika mataji hayo 13 ambayo Yondani amefanikiwa kutwaa, manane akiwa na Yanga, manne akibeba alipokuwa Simba na taji moja ambalo ametwaa na timu ya Taifa ni lile la Cecafa Chalenji.

Pia ameshiriki mara mbili katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na Yanga lakini pia amefanikiwa kucheza Fainali za Afrika (Afcon) na zile za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).

 

Mti mkavu Taifa Stars

Kati ya wachezaji walioitumikia kwa muda mrefu zaidi timu ya taifa ya Tanzania, Yondani ni mmojawapo ambapo amecheza kwa miaka 11.

Katika kipindi hicho chote, Yondani amekuwa ni nguzo imara ya timu hiyo katika mashindano mbalimbali ambayo imekuwa ikishiriki.

Beki huyo ameweka rekodi ya mchezaji aliyeshiriki mashindano ya Chalenji mara nyingi ambapo amefanya hivyo mara nane.

 

Siri ya mafanikio

Yondani anafichua kuwa siri ya mafanikio yake ni kujituma na kufuata vyema maelekezo ambayo amekuwa akipewa na benchi la ufundi la Yanga.

“Kwa mchezaji hakuna cha ziada ambacho kinaweza kukufanya uwe bora zaidi ya kujituma na kutimiza majukumu yako uwanjani.

Unatakiwa uwe fiti na unapocheza ucheze kwa umakini wa hali ya juu kwani vinginevyo utakutana na wapinzani ambao wako vizuri halafu utashindwa kuwadhibiti.