Mzee Kichuya afunguka ishu ya mwanae

BABA mzazi wa winga wa Simba, Shiza Kichuya, mzee Ramadhani Kichuya ameshangazwa na uamuzi wa mwanaye kuacha kucheza soka la kulipwa nchini Misri na badala yake kurejea timu yake ya zamani.
Simba imemsajili Kichuya wakati wa dirisha dogo la usajili ingawa hadi sasa hajacheza mechi hata moja ya Ligi Kuu na tangu asajili Simba imecheza mechi mbili dhidi ya Mbao FC na Alliance FC zote za jijini Mwanza na walishinda.
Jana Jumamosi, Simba ilicheza mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo winga huyo hakucheza.
Sababu za Kichuya kutocheza mechi hizo ni kutopatikana kwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kutoka Misri ambapo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema wana mpango wa kuomba msaada FIFA ili hati hiyo ipatikane kwani kuna ugumu kutoka klabu aliyokuwa akiitumikia Misri na shirikisho lao.
Simba ilimuuza Kichuya klabu ya ENPPI inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri ambao, walimtoa kwa mkopo katika timu ya Pharco FC zote za nchini humo.
Mzee Kichuya aliliambia Mwanaspoti kuwa, mwanaye huyo hajamshirikisha katika uamuzi huo ingawa anaona alichokifanya si uamuzi sahihi kwani anarudi nyuma badala ya kusonga mbele kisoka.
“Sifahamu hata huko Simba amesaini mkataba wa muda gani, maana hajanishirikisha kwa lolote lakini kwasababu naelewa mpira mwanangu hapo ameteleza, alipaswa kukomaa huko huko nje na sio kuanza safari upya, kiukweli hajautendea haki mpira.
“Sijui huko alikokuwa kulikuwa na shida gani, ni mazingira ama kiwango chake sielewi ameniacha nafikiria sababu hasa za kumrudisha hapa tena kucheza ambapo nilijua mwanangu ameanza safari ya mafanikio kutimiza ndoto yake.
“Kurudi kucheza soka hapa nchini ni kujirudisha nyuma kisoka na bahati huwa haiji mara mbili, hivyo safari yake ya kucheza soka la kulipwa inaweza kuwa na changamoto. Lakini, kwa kuwa kuna wakala mambo yanaweza kubadilika…tusubiri,” alisema mzee huyo ambaye aliripotiwa kuwa katika mivutano na kifamilia na mwanaye huyo.