Mzee Kilomoni, Ndolanga, Kipingu wafunguka sakata la Mo Dewji

Muktasari:

  • Mo Dewji kupitia ukarasa wake wa twitter aliandika kujiuzulu wadhifa huo muda mfupi baada ya Simba kuruhusu kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi juzi usiku visiwani Zanzibar.

Dar es Salaam. Aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba, Hamis Kilomoni na mwenyekiti wa zamani wa FAT sasa TFF, Muhidin Ndolanga wamezungumzia kitendo cha Mfanyabiashara, Mohamed Dewji (Mo Dewji) kutangaza kujiuzuru unatokana na mfumo wa uwekezaji ndani ya klabu ya Simba.

Mo Dewji alizua taharuki kwa wadau wa soka nchini kufuatia tamko lake la kutangaza kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa klabu ya Simba kabla ya kutengua kauli ndani ya saa chache kwenye mtandao wa kijamii.

Akizungumzia sakata hilo Mzee Kilomoni alisema tatizo lililopo ni kumtegemea mtu mmoja ndani ya klabu, jambo ambalo si zuri.

 “Mo (Dewji) naye ni binadamu kuna muda anataka apate kitu fulani kwa hiyo asipopata anaangalia hiko kitu kina umuhimu gani, inawezekana aliangalia hilo ndiyo sababu akatangaza kujiuzulu awali.

Kilomoni alisema Simba imeweza kujiendesha kwa zaidi ya miaka 80 ikiwa chini ya wananchi hivyo wanapaswa kutambua hata asipokuwepo Mo Dewji, klabu itaendelea kujiendesha.

Naye Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF), Muhidin Ndolanga alisema suala la uwekezaji ndani ya klabu ni ngumu na inachukuliwa tofauti.

Ndolanga ambaye ni rais wa heshima wa TFF, alisema tafsiri ya uwekezaji ilivyo nchini ni tofauti na yeye anavyoelewa, ingawa amedai hawezi kuzungumzia matamko ya Mo Dewji na Simba ya juzi na jana.

“Ila kuna siku nitamuomba rais TFF na Mwenyekiti BMT tufanye kikao cha ndani juu ya uwekezaji ndani ya klabu zetu za soka, kinachofanyika ni tofauti na uhalisia,” alisema Ndolanga.

Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Iddi Kipingu alisema hizi timu zetu za Simba na Yanga ukishakuwa mpenzi, mwanachama au hata shabiki, kasha ukasema unajitoa ni uongo na ndicho kimemkuta Mo.

Kipingu alisema tamko lake la awali la kujitoa anafikiri lilichangizwa na mihemko ya kibinadamu kama itakavyomtokea mtu mwingine kwa kutarajia kupata kitu fulani kisha akakikosa.

Alisema anadhani uamuzi wa awali ulikuwa wa jazba ambazo baada ya kutulia amelazimka kurejea na anatarajia haitotokea tena Mfanyabiashara huyo kutoa tamko la kujiuzulu kwani katika maisha umri unaposogea ndipo unazidi kuwa mvumilivu na ndivyo itakuwa kwa Mo Dewji ndani ya Simba.

Mo Dewji kupitia ukarasa wake wa twitter aliandika kujiuzulu wadhifa huo muda mfupi baada ya Simba kuruhusu kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi juzi usiku visiwani Zanzibar.

Katika ukurasa huo, Mo Dewji aliandika kujiuzulu nafasi hiyo na kusema atasalia kuwa mwekezaji ndani ya klabu ya Simba, akibainisha kwamba ametumia Sh 4 Bilioni kulipa mishahara kwa mwaka lakini timu hiyo imekuwa ikipata matokeo ya aibu, hivyo atasalia Simba kama mwekezaji na kuwekeza katika soka la vijana, ujumbe ulioibua taharuki.

Hata hivyo saa chache baada ya ujumbe huo wa juzi usiku, jana saa 6 mchana, Mfanyabiashara huyo kupitia ukurasa wake wa twitter alisema bado yupo na ataendelea kuwepo Simba, kitendo kilichoibua mjadara.

Aliandika: “Kilichotokea jana katika akaunti yangu ni kwa bahati mbaya, tuko pamoja  na tunarudi kwenye Ligi kwa ubora na tunajipanga, Nawapongeza Mtibwa kwa kuchukua kombe.”

 “Mimi ni Simba damudamu, nitabaki kuwa Simba,” ali-twiti Mfanyabiashara huyo na mwekezaji wa klabu ya Simba.

Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda alisema hajui taarifa za kutangaza kujiuzulu Mo Dewji na anachokifahamu bado ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ndani ya klabu hiyo.

Kauli sawa na iliyotolewa na Mkurugenzi mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu, Senzo Mazingisa ambaye awali alisema hawajapata taarifa rasmi.

Siwezi kusema itakuaje akiondoka kwasababu hakuna kitu kama hicho, hizo taarifa mimi mwenyewe nimeziona kama wewe kwahiyo sio kitu rasmi,” alisema Mazingisa.