Nado, Domayo, Chilunda, Sure Boy waachwa Kilimanjaro Stars, Manula atia neno

Muktasari:

Mashindano ya Cecafa Chalenji yatafanyika Uganda kuanzia Disemba 7 hadi 19 katika jiji la Kampala.

Dar es Salaam. Wachezaji wanne wa Azam FC, viungo Frank Domayo na Salum Abubakar 'Sure Boy' pamoja na washambuliaji Shaban Chilunda na Iddi Seleman 'Nado' wameenguliwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Bara kutokana na kuwa majeraha.

Kilimanjaro Stars ipo Kundi C pamoja na Kenya, Zanzibar na Djibout katika mashindano ya Chalenji yatakayofanyika jijini Kampala, Uganda kuanzia Jumamosi ya wiki hii.

Akizungumza jijini leo, Daktari wa Kilimanjaro Stars, Emil Urassa alisema wachezaji hao wameshindwa kupona majeraha yao kwa wakati hivyo benchi la ufundi limewaondoa katika hesabu yake.

"Salum Abubakar ameliripoti kambini, lakini alikuwa tayari na majeruhi aliyoyapata katika mchezo wa Azam na JKT Tanzania, pia Chilunda naye alionekana ana majeraha ambayo aliyapata katika mchezo wa mwisho wa timu yake.

“Iddi Seleman yeye aliumia katika mazoezi ya jana na Frank Domayo huyu aliumia kabla hata ya kujiunga na timu ya taifa," alisema Dokta Urassa.

Kwa upande wake kocha mkuu wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda alisema vijana wake wako tayari kwa mashindano hayo.

"Tunajiandaa kwenda kushindana katika mashindano ya Chalenji kwa hiyo yoyote ambaye tutakutana naye sisi tuko tayari kucheza naye.

Mimi na benchi langu la ufundi tumejiandaa vizuri kwenda kukabiliana na ushindani na mwisho wa yote tuweze kupata matokeo mazuri," alisema Mgunda

Kipa Aishi Manula alisema kuwa ndoto ya kikosi cha Kilimanjaro Stars ni kutwaa ubingwa

“Tunaelewa nia na madhumuni ya mashindano haya na lengo letu kama nchi kwamba ni kwenda kufanya vizuri. Ukiangalia ni muda mrefu umepita bila kutwaa taji hili hivyo sisi kama wachezaji tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi ili tuweze kuitangaza vyema nchi yetu.