Nafasi ya Stars Chan iko hapa

Dar es Salaam. Kucheza kwa nidhamu, umakini na kujituma uwanjani ndiyo mambo yatakayoivusha Taifa Stars katika mchezo wa leo dhidi ya Sudan wa kusaka nafasi ya kufuzu kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).

Mshindi wa jumla katika mchezo huo atafuzu fainali hizo zitakazopigwa nchini Cameroon mwakani, Taifa Stars itacheza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kurudiana Sudan Oktoba 18.

Taifa Stars ilifuzu fainali hizo mara ya kwanza mwaka 2009 na kuishia hatua ya makundi wakati Sudan imeshiriki mara mbili na zote ilitwaa medali ya shaba.

Sudan ilifuzu mara ya kwanza 2011 na kumaliza nafasi ya tatu ikiwa mwenyeji ambapo Tunisia ilitwaa ubingwa kwa kuilaza Angola mabao 3-0 katika mchezo wa fainali.

Ilishiriki tena 2018 na kutwaa medali ya shaba ilipomaliza nafasi ya tatu, baada ya kuifunga Libya penalti 4-2 ilipopata matokeo ya sare ya bao 1-1 huku wenyeji Morocco wakitwaa ubingwa kwa kuifunga Nigeria katika fainali.

Wakati nyota wengi wa Taifa Stars wanatokea Simba, Yanga na Azam, kwa Sudan ni Al-Hilal, Al-Merrikh, Al-Ahly, El-Hilal, Al-Ahli na Al-Khartoum.

Kauli za makocha

Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda alisema wamejiandaa kwa kiwango bora na wamefanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika mechi dhidi ya Kenya na Burundi.

“Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije aliweka programu maalumu naomba Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kufanya timu kuwa na wachezaji 12,” alisema Mgunda.

Kocha wa Sudan, Zdravko Logarusic alisema wanaiheshimu Taifa Stars kwa kuwa ina kikosi imara, hivyo anatarajia kupata ushindani mkubwa na hawezi kutambia rekodi ya Sudan kwa kuwa soka imebadilika.

Rekodi

Rekodi haziibebi Tanzania, hivyo Taifa Stars italazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha inasonga mbele.

Tangu mwaka 1967, Tanzania na Sudan zimekutana mara 23, Sudan imeshinda mechi 11, Taifa Stars nne na sare nane.

Katika mechi 10 zilizopita, Taifa Stars imepata ushindi mara moja, imepoteza mechi tano dhidi ya Sudan na zimetoka sare michezo minne.

Ushindi huo mmoja katika mechi 10 zilizopita, ulikuwa ni wa mabao 2-0 katika michuano ya Cecafa Novemba 25, 2012.

Ushindi mkubwa ambao Taifa Stars imewahi kupata dhidi ya Sudan ni 3-0 katika mechi ya kirafiki Julai 4, 1972, wakati ushindi mkubwa waliopata Sudan dhidi ya Tanzania ni 3-0 katika mechi ya kirafiki Januari 10, 1969.

Katika mechi 15 zilizopita za michuano mbalimbali, Tanzania imeshinda mara tano imefungwa sita na sare nne huku ushindi mnono zaidi ukiwa ni 3-0 dhidi ya Uganda Machi 24, 2019

Katika kufuzu kwa fainali za Afcon. Vipigo vikubwa zaidi ilivyopata Taifa Stars katika mechi hizo 15 vilikuwa ni mabao 3-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 12, 2018 katika kufuzu Afcon na 3-0 dhidi ya Algeria katika fainali za Afcon 2019 nchini Misri.

Sudan katika mechi zao 15 zilizopita za michuano yote imeshinda saba imepoteza sita na sare mbili, katika hizo ushindi mkubwa walipata ni 3-1 dhidi ya Chad katika mechi ya mwisho waliyocheza ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia Septemba 5, 2019. Kipigo kikubwa walichopata Sudan katika mechi 15 ni mabao 4-1 dhidi ya Equatorial Guinea Machi 22, 2019 kuwania kufuzu kwa Afcon.

Kwa mujibu wa viwango vya ubora wa soka duniani vya Fifa, Tanzania inashika nafasi ya 135 baada ya kupanda kwa nafasi mbili wakati Sudan iko nafasi ya 128 baada ya kupanda kwa nafasi moja.

Mchezaji wa kuchungwa

Mshambuliaji Saifeldin Bakhit wa Al-Merrikh ndiye tegemeo la kocha wa zamani wa Simba, Mcroatia, Logarusic ambaye anakinoa kikosi cha Sudan tangu 2017.

Bakhit amefunga mabao tisa katika mechi 10 za mwisho, amefunga manne na mengine yakifungwa na Yasir Mozamil wa Al-Ahly, kiungo Mohamed Mokhtar wa Al-Hilal, Khalid Abdelmoneim wa Al-Merrikh na kiungo Mofadal Mohamed wa El Hilal.

Hiyo ni ishara mabeki Taifa Stars chini ya wakongwe Kelvin Yondani na Erasto Nyoni wanapaswa kuwa makini.

Wadau walonga

Kocha wa Prisons, Mohamed ‘Adolf’ Rishard alisema endapo Taifa Stars itacheza kwa umakini, ina nafasi ya kucheza Chan.

“Walipotoka sare na Kenya niliona nafasi yao ya kufanya vizuri ipo japo kuna watu waliona sare nyumbani tumepoteza,”alisema.

Mchambuzi Ally Mayay alisema Sudan sio timu nyepesi, lakini kama Taifa Stars itaweka nia ya kushinda, nafasi ya Tanzania kufuzu Chan ipo.

CAMEROON 2020

Nchi 48 (kati ya 53) wanachama wa CAF ziliingia katika mbio za kuwania nafasi 16 za kufuzu Chan 2020.

Timu 16 zitashiriki fainali za Chan 2020 ambazo nafasi za kufuzu zimegawiwa kwa kanda. Katika timu sita zilizobaki Cecafa, mbali na Tanzania na Sudan zinawazowania nafasi moja ya kufuzu, nafasi nyingine mbili zitawaniwa na Burundi ambao jana ilivaana na Uganda wakati Ethiopia ilichuana dhidi ya Rwanda.