Namungo yaikomalia Yanga, yaanza kushona sare

Dar es Salaam. Yanga imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Tariq Seif kabla ya wenyeji Namungo kusawazisha kipindi cha pili kupitia Bigirimana Blaise.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kubaki nafasi ya tatu ikiwa na pointi 51, wakati Namungo ikiwa ya nne na pointi 50, huku Simba ikiongoza kwa pointi 71, ikifuatiwa na Azam (54).
Katika mchezo huo Yanga iliyoongozwa na kocha msaidizi, Charles Mkwasa kutokana na kocha wake Mbelgiji Luc Eymael kutumikia adhabu ya kadi mbili za njano na kutakiwa kukaa jukwaani.
Mshambuliaji Tariq akiwa amepona majeruhi yake alifungia Yanga bao la kuongoza katika dakika 6, kupitia akiunganisha kwa kichwa krosi ya Juma Abdul na kumwacha kipa wa Namungo, Nouridine Barolana akiwa hajui la kufanya.
Baada ya kufunga bao hilo, Tariq alikimbia nje na kumtafuta Andrew Dante na kugonga naye tano kadhaa kwa ngumi na kuendelea kushangilia na wachezaji wengine.
Safu ya ulinzi wa Yanga kwa mara ya kwanza mabeki wa kati walicheza Juma Said 'Makapu' na  Ally Mtoni 'Sonso' wakichukua nafasi za Kelvin Yondani au Mghana Lamine Moro hawakuwepo kabisa kutokana na sababu ya maumivu na matatizo ya kifamilia.
Kipenzi cha mashabiki wa Yanga, Mghana Bernald Morrison ambaye aliukosa mchezo wa KMC iliyowachapa bao 1-0, alicheza winga ya kulia na kuing'arisha safu yake ya ushambuliaji iliyokuwa na Tariq, Patrick Sibomana na Ditram Nchimbi.
Yanga walicheza kwa kujiamini kipindi cha kwanza mbali na bao la Tariq lililofungwa dakika ya sita, mshambuliaji huyo alipiga shuti kali kinyume dakika ya 20, likatoka nje.
Kipindi cha pili Namungo iliingia kwa nguvu na kufanikiwa kusawazisha bao katika dakika ya 62, lililofungwa kwa kichwa na Bigirimana.
Washambuliaji wa Namungo, Abeid Athuman, Lucas Kikoti na Hashim Manyanya walikuwa moto katika kufanya mashambulizi.
Mkwasa alifanya mabadiliko kwa kuwatoa, Sibomana akaingia Mapinduzi Balama, Tariq kwa Deus Kaseke na Muivory Coast Yikpe Gislain kwa Nchimbi lakini hayakuleta matunda.
Dakika chache kabla mpira kuisha Yanga walibadili staili na kucheza mipira mingi mirefu na dakika ya 84, Kaseke alipiga shuti likatoka nje.
KMC yaifanya ngazi Alliance
Uwanja wa Uhuru, mshambuliaji Charles Ilanfya alifunga mabao mawili wakati KMC ikishinda 2-1 dhidi ya Alliance FC.
Huo ni ushindi wa pili mfululizo wa KMC baada ya katika ta wiki kuichapa Yanga na kujiweka katika mazingira mazuri ya kukimbia janga la kushuka daraja msimu huu.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa wenyeji KMC walikuwa mbele kwa bao lililofungwa na Ilanfya dakika ya 44 baada ya safu ya ulinzi ya Alliance kuzembea kutoa mpira eneo la hatari.
Zikiwa zimesalia dakika nne mchezo kumalizika, Ilanfya alifunga bao pili kwa KMC kabla ya wageni Alliance kupata bao la kufutia machozi lililofungwa dakika ya 90 na Michael Chenudu.
Timu hizo mbili zipo kwenye hatari ya kushuka daraja kutokana na nafasi wanazoshika kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ambao Alliance inasalia nafasi ya 18 na alama zake 29 huku, KMC ikipanda nafasi moja hadi nafasi ya 15 kwa alama zao 33.
Kocha wa Alliance, Fredy Felix 'Minziro' alisema tatizo bado kubwa kwa timu yake kufuata maelekezo anayowapa wakati wa mazoezi.
Hererimana Haruna wa KMC alisema ushindi huo unaongeza matumaini ya kuendelea kubaki Ligi Kuu msimu ujao kama watakuwa na mwenendo mzuri katika michezo inayofuata.