VIDEO: Ndairagije asaini miaka miwili, apewa jukumu zito Azam

Muktasari:

  • Azam ni bingwa mtetezi wa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) sambamba na Kombe la FA na msimu ujao itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Dar es Salaam. Uongozi wa Azam FC umetaja vipaumbele vyake viwili kwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo Etienne Ndairagije leo amesaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu hiyo.

Ndairagije ameingia mkataba huo na Azam kuziba pengo la Mholanzi Hans Pluijm aliyetimuliwa katikati mwa msimu uliopita kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' alisema wanaamini kocha huyo atawapa mataji pamoja na kuendeleza mfumo wa soka la vijana.

"Kwa niaba ya bodi ya timu, nachukua fursa hii kumkaribisha kocha Etienne. Tumefanya utafiti wa kutosha tukabaini kuwa yeye ni mtu sahihi wa kuwa kocha mkuu wa Azam.

Kikubwa ni kwamba sisi kipaumbele chetu ni kupata kila kombe tunaloshiriki na ndio maana huwa tunafanya vizuri hata kwenye Kombe la Mapinduzi, lakini pia ni kocha ambaye anatoa fursa kwa vijana," alisema Popat.

Ndairagije alisema anafurahia kujiunga na klabu hiyo na kutamba kuwa hana presha yoyote.

"Nashukuru uongozi wa Azam kwa kuniamini. Jambo la faraja kwetu kwao kutuamini kwa sababu ni ndoto ambayo tumekuwa nayo kwa ajili ya kuendeleza taaluma yetu.

“Kwanza ni kuhakikisha kazi ambayo imeanzishwa na klabu inakuwa bora zaidi. Kazi yetu ya ukocha kila siku ina changamoto mpya na inahitaji ubunifu na ni jambo la kawaida kwa kocha kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine," alisema Ndairagije.