Ndayiragije afungasha virago Azam njiani kutua Stars

Muktasari:

Ndayiragije alijiunga na Azam FC mwanzoni mwa msimu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea KMC na leo anatarajia kuachana na timu hiyo akiwa ameipa ushindi kwenye michezo mitatu ya ligi waliyocheza.

Dar es Salaam.Uongozi wa Azam FC, leo unatarajia kumuaga rasmi aliyekuwa kocha wao Ettiene Ndayiragije anayetarajia kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa 'Taifa Stars'.

Leo saa 8 mchana Azam watamuaga kocha huyo na kumtambulisha aliyekuwa kocha wao wa zamani Aristica Cioaba aliyewasili jijini jana usiku tayari kwaajili ya kujiunga na waajili wake hao wa zamani.

Chanzo cha kuaminika kimeliambia Mwanaspoti kuwa, mchana wa leo watakuwa na sherehe ndogo ya kumuaga Ndayiragije na kumkaribisha Cioaba tayari kwaajili ya majukumu ya kukinoa kikosi hicho.

"Baada ya makubaliano kati ya Ndayiragije na uongozi wa Azam FC kuamua kuvunja mkataba na aliyekuwa kocha wao ambaye anatajwa kukinoa kikosi cha Stars sasa leo mchana wanatarajia kumuaga na kumtakia majukumu mema huko anakotarajia kwenda,".

"Cioba yupo kawasili tangu jana usiku tuponaye atakuwepo katika tafrija hiyo ya kuagwa kwa Ndayiragije na yeye kupewa majukumu mapya kwa kukabidhiwa ripoti alipoishia kocha anaeondoka ili kuendeleza pale alipoishia na timu iendelee kupata matokeo," akidai chanzo hicho.