Ndayiragije amchomoa Mkude kambini Taifa Stars

Muktasari:

  • Mkude alitoa taarifa kwa Kocha Ndayiragije akiomba ruhusa kuondoka kambini ili kwenda kushughulikia masuala yake ya kifamilia

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amempa ruhusa kiungo Jonas Mkude kuondoka katika kambi hiyo kwenda kushughulikia masuala yake ya kifamilia yanayomkabili.

Taarifa iliyotolewa na Afisa Habari na Mawasiliana wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo ilisema, Mkude alitoa taarifa kwa Kocha Ndayiragije akiomba ruhusa kuondoka kambini ili kwenda kushughulikia masuala ya kifamilia, ruksa ambayo alipewa tangu Jumamosi ya wiki iliyopita kabla ya kambi kuanza.

Jana Jumatatu Mkude, aliripoti kambini na kumweleza Kocha Ndayiragije kuwa bado hajamaliza masuala anayosughulikia, hivyo kocha ameamua kumpa ruhusa ya kwenda kumaliza suala lake.

Taarifa hiyo ilieleza, kulingana na kuwepo muda mfupi kuelekea mchezo dhidi ya Equatorial Guinea, Kocha Ndayiragije hataweza kuongeza mchezaji mwingine.

Taifa Stars itajitupa Uwanja wa Taifa Ijumaa wiki hii katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi kusaka tiketi ya kushiriki Afcon 2011 Cameroon na baada kusafiri hadi Tunisia kwenda kucheza dhidi ya Libya.