Advertisement

VIDEO: Ndo katua sasa !

Friday October 16 2020

KOCHA mpya wa Yanga, Mrundi Cedrick Kaze usiku wa kuamkia leo Ijumaa alitua kwenye ardhi ya Dar es Salaam tayari kuanza kibarua chake Jangwani.

Kaze, ambaye Kocha wa zamani wa timu za vijana za Burundi za miaka 17, 20 na 23 na ile ya wakubwa, aliiambia Mwanaspoti ametua kamili kwa kupiga mzigo na ana vipaumbele vyake muhimu ili kujenga timu imara.

Mrundi huyo aliyefanya kazi kwenye akademi za Barcelona, ambaye Mwanaspoti lilikuwa la kwanza kufichua ujio wake Yanga, jana alizungumza moja kwa moja wakati anaanza safari kutoka Canada hadi anatua Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro kisha saa 4 usiku akashuka Dar akiwa ndani ya KLM.

Kaze akionekana mwenye mzuka aliiambia Mwanaspoti kuwa, anafahamu kila kinachoendelea ndani ya Yanga na alikuwa na mawasiliano ya karibu sana na wasaidizi wake Juma Mwambusi na Vladmir Niyonkuru.

Kocha huyo ambaye atatambulishwa rasmi leo kambini kwa wachezaji na viongozi wengine, alisema: “Najivunia kuwa kocha mpya wa Yanga yenye historia, timu yenye mashabiki wa aina yake na miongoni mwa timu bora za Afrika.”

Alisema anatambua kiu ya mashabiki wa Yanga na anaamini akipata ushirikiano wa kutosha kama anavyofikiria, basi wasubiri makubwa ndani ya muda mfupi huku kibarua chake cha kwanza kikiwa dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Mkapa Alhamisi ijayo kama atakuwa amepata vibali vya kazi. Baada ya mechi hiyo, atakwenda ugenini kule Mwanza dhidi ya KMC kisha Musoma dhidi ya Biashara ambayo huwa haitaki masihara ikiwa uwanja wake.

Advertisement

Lakini, Kaze ambaye ni mzoefu amewaambia Yanga kuwa kwa aina ya timu iliyosajiliwa anaamini kazi itafanyika kwa kiwango cha juu na mafanikio yatapatikana.

Alisema ana uelewa mzuri wa wachezaji wengi wazawa na wale wa kigeni ambao, asilimia kubwa amewapendekeza yeye kipindi alichokuwa akitakiwa na Yanga kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Zlatko Krmpotic aliyetimuliwa kazi.

Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti alisema; “Nimeangalia mechi zote za ligi tangu ile ya Prisons mpaka hii ya mwisho ya Coastal tuliposhinda mabao 3-0, nimeangalia pia na mechi za timu zingine ikiwemo Simba, Azam, Namungo, Polisi na timu karibu zote. Nimewaangalia kupitia Azam, nimeona levo yetu na wapinzani wetu, nimeona viwanja vya Dar es Salaam na mikoani sasa naweza kusema nina picha halisi ya kila kitu ninachokuja kufanya, nimeshuhudia mpaka mechi za kirafiki, nakuja kuanza kazi sehemu ambapo najua kila kitu.

“Nashukuru viongozi wamefanya usajili mzuri sana na sio kusema kuwa hakuna sehemu ya kurekebisha, lakini timu hii ni nzuri sana. Hata ukiangalia mechi na Coastal ni watatu tu walicheza ambao walikuwa msimu uliopita, hapo maana yake ni kwamba asilimia 80 ya timu ni mpya na muda unakwenda. Tunahitaji kushinda na kuijenga timu.”

“Nataka timu yangu imiliki mpira, icheze mpira, itengeneze nafasi. Nataka timu yangu itawale uwanja, nataka wakati tunacheza timu yangu iwe mbali na goli langu.

“Sichezeshi wachezaji 11 bora uwanjani nachezesha timu bora uwanjani.Sichezeshi jina wala staa, nachezesha timu ambayo italeta mafanikio na usishangae mchezaji mkubwa akawa anakaa benchi. Tunaangalia timu zaidi,” alisema.

Advertisement