Ndugai: Lishe duni ya wachezaji wetu imechangia Stars kufungwa

Muktasari:

  • Taifa Stars ilipoteza mchezo wa kwanza kwa kufungwa mabao 2-0, dhidi ya Senegal kwenye Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema miongoni mwa sababu iliyochangia Stars kupoteza mchezo wa kwanza jana dhidi ya Senegal ni lishe duni ya wachezaji wetu.

Spika Ndugai ameyasema hayo muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam akitokea Misri aliposhuhudia mchezo wa kwanza wa Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Senegal na Tanzania uliomalizika kwa Taifa Stars kuchapwa 2-0.

Ndugai alisema ukiangalia kwa umakini utaona wale wachezaji wa timu pinzani walikuwa na miili mizuri ambayo inatokana na lishe nzuri.

"Kuna umuhimu wa kuwapa wachezaji wetu lishe nzuri ya kutosha ili kushindana na wapinzani wa aina ya Senegal," alisema Ndugai.

Katika hatua nyingine Ndugai alisema viongozi wengi wa soka na michezo mingine hapa nchini siyo watu sahihi wa kuongoza.

Ndugai aliungana na wabunge wengine kwenda Misri kuwapa morali wachezaji na makocha wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) alisema Watanzania tumeachia michezo kama ni vile mtu yoyote anaweza kuongoza kitu ambacho siyo sahihi na kuna ulazima wa kuanza mchakato kupata viongozi hao wazuri.

"Wakipatikana viongozi wazuri wataweza kuongoza klabu zetu mbalimbali mpaka vijijini huko, wilayani na mikoani," alisema.

"Tunatakiwa kuondoa rushwa katika michezo ili kupiga hatua kwani ni miongoni mwa sehemu inayoturudisha nyuma katika michezo mingi na kushindwa kufanya vizuri," alisema Ndugai.